MAONESHO YA PILI YA SIDO KITAIFA 2019 YAFANA MKOANI SINGIDA

Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) likishirikiana na  ofisi ya mkuu wa mkoa wa Singida ilifanya maonesho ya  pili ya  SIDO - kitaifa yaliyojumuisha wajasiriamali  kutoka  mikoa yote ya Tanzania bara pamoja na nchi jirani za Kenya, Uganda na Burundi. Maonesho hayo yalifanyika katika viwanja vya Bombadier  mkoani Singida kuanzia tarehe 4 /10 hadi 9/10 /2019  yakiwa na kauli mbiu ya maonesho hayo yalikuwa “Teknolojia bora na bunifu kwa viwanda vidogo na vya kati ni nguzo bora ya uchumi endelevu”.

Maonesho hayo yalifunguliwa rasmi na Waziri Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa Kassim (MB) tarehe 7/10/2019. Katika hotuba yake, Waziri Mkuu aliupongeza uongozi wa SIDO kwa kazi nzuri ya  kubuni na kuratibu maonesho ya SIDO kitaifa na Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa kukubali kuwa  mwenyeji kwa kushirikiana na SIDO katika kufanikisha maonesho.  Aidha alifurahishwa kwa kuona  teknolojia mbalimbali za mashine zikiwemo  mashine za kusindika, kuchakata na kusaga bidhaa mbalimbali ambazo zitaongeza  dhamani   katika maligafi/ mazao  yetu pamoja na  bidhaa nyingi zikiwa na  ubora  na viwango vinavyotakiwa.

Alisisitiza kuwa ubunifu unaoonyeshwa na SIDO ndiyo ubunifu unaopendekezwa na serikali ya awamu ya tano.  Aliwaasa wajasiriamali  wazidi  kushiriki kwa wingi maonesho yanayoandaliwa na SIDO kwa kuwa ndiyo  fursa kubwa ya kutangaza   bidhaa zao ili ziweze  zinajulikana ndani na nje ya nchi,  fursa ya  kukutana na wataalamu mbalimbali,  kupata miadi ya bidhaa zao, kupata mirejesho kuhusu changamoto za bidhaa zao, kupata technolojia bora zaidi, kupanua wigo wa ushirikiano na sekta binafsi, kudadisi kuhusu taaasisi zinazotoa huduma mbalimbali kwa wajasiriamali ikiwemo elimu n.k. Mhesimiwa Waziri Mkuu alizitaka benki mbalimbali hapa nchini kuwawezesha wajasiriamali ili waweze kukuza biashara zao kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu. 

Aidha waziri alisema kuwa maonesho haya yameondoa  imani potofu kuwa, kitu bora ni kutoka nje . Aliongeza kuwa, bidhaa zetu ni bora na zina viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa kwa kuwa zimedhibitishwa  na shirika linalotambulika kimataifa yaani Shirika la Viwango Tanzania (TBS).  Waziri alisema kuwa ipo haja ya kuangalia namna ya kuzipa kipaumbele bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na kuweka mikakati ya kuziwesesha kupata  masoko ya uhakika. Aliwataka wadau mbalimbali kuweza kuwekeza hapa nchini na uwekezaji huo uzingatie ubora na uendelevu.

Maonesho hayo yalifungwa rasmi tarehe 9/10/2019 na Waziri wa Viwanda na Biashara,  Mheshimiwa Innocent Bashungwa.