Maonesho ya Kimataifa ya Dar Es Salaam yamejijengea sifa kwa miaka mingi kama dirisha kuu la kuonesha bidhaa za Tanzania pamoja na nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika. Ikiungwa mkono na huduma za Bandari ya Dar es Salaam inayohudumia ukanda huu kwa ufanisi, maonesho haya hufanya kazi kama kituo kimoja (one-stop centre) cha kufikia masoko ya nchi mbalimbali ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi, Zimbabwe na Botswana.
Maonesho haya hupata ushiriki mkubwa kutoka kwa wafanyabiashara wa Tanzania ambao hushiriki kama waoneshaji na pia hutumia jukwaa hili kwa kubadilishana uzoefu na kufanya biashara. Ushiriki umeendelea kuongezeka kwa kasi kutoka zaidi ya kampuni 100 mwishoni mwa miaka ya 1980 hadi kufikia kampuni 1,041 mwaka 1999. Mwaka 2006, jumla ya waoneshaji 1,526 walishiriki, wakiwemo washiriki kutoka nchi zaidi ya 26 duniani, Tanzania ikiwemo.
Kwa sasa, maonesho haya ni miongoni mwa maonesho makubwa zaidi barani Afrika, yakikusanya zaidi ya kampuni za ndani 3,500 na zaidi ya kampuni 200 za kimataifa, huku nchi 26 zikishiriki katika maonesho ya mwaka 2025.

