UJASIRIAMALI HAUNA UMRI! SIDO TANGA YAWAJENGEA WATOTO, VIJANA NA WAZEE UJUZI WA UJASIRIAMALI NA UZALISHAJI
Imewekwa: 23 Nov, 2026
UJASIRIAMALI HAUNA UMRI! SIDO TANGA YAWAJENGEA WATOTO, VIJANA NA WAZEE UJUZI WA UJASIRIAMALI NA UZALISHAJI

Ujasiriamali hauna umri!  Huu ndio ujumbe unaotolewa na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Mkoa wa Tanga, kupitia mkakati wake wa kupanua wigo wa mafunzo ya ujasiriamali na ujuzi wa uzalishaji kwa watu wa rika zote, bila kuweka mipaka ya umri katika kujifunza na kukuza uwezo wa kiuchumi.

Ujumbe huu umedhihirika kupitia mafunzo ya utengenezaji wa sabuni na vipodozi yanayofanyika kuanzia tarehe 16 hadi 20 Novemba 2026, ambapo darasa limewakutanisha washiriki wa rika mbalimbali, wakiwemo watoto sita wenye umri chini ya miaka 12 pamoja na wazee.

Ushiriki wa watoto katika mafunzo haya ni hatua muhimu katika kuwajengea msingi wa ujasiriamali tangu wakiwa wadogo. Kupitia mafunzo ya vitendo, watoto wanapata fursa ya kugundua vipaji vyao, kukuza ubunifu, kujenga kujiamini na kujifunza misingi ya uzalishaji na ujasiriamali. Hatua hii inalenga kuandaa kizazi chenye fikra bunifu, uwezo wa kutatua changamoto na utayari wa kujiajiri na kujitegemea kiuchumi hapo baadaye.

Kwa upande mwingine, ushiriki wa vijana, watu wazima na wazee unaonesha kuwa kujifunza ujuzi mpya na kuanzisha shughuli za kiuchumi si jambo linalofungamana na umri. Kila mtu ana nafasi ya kujifunza, kuboresha uwezo wake na kutumia ujuzi alionao kujenga au kukuza shughuli za uzalishaji na biashara.

Kupitia mkakati huu, SIDO Tanga inalenga kujenga jamii yenye utamaduni wa ujasiriamali, ambapo watoto wanajengewa misingi ya ubunifu na ujasiriamali tangu utotoni, vijana wanawezeshwa kujiajiri, huku watu wazima na wazee wakipata fursa ya kuongeza ujuzi, kuboresha bidhaa na kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.

Kwa SIDO Tanga, umri si kikwazo cha kujifunza, kubuni wala kufanya biashara. Kila mtu ana uwezo wa kujifunza ujuzi mpya, kuanzisha shughuli ya uzalishaji na kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya familia na taifa.

Ujasiriamali unaanza pale mtu anapopewa fursa ya kujifunza!

 

 

Matangazo
03 Dec, 2025
23 Nov, 2025
Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo