Serikali emeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kukuza uchumi wa wananchi kwa kufungua milango ya biashara kupitia maonesho ya kimataifa ya 11 ya ‘AGROFOOD PLASTPACKPAPER AFRICA 2026’ yaliyofanyika kuanzia tarehe 29 hadi 30 Januari, 2026 katika ukumbi wa Diamond Jubilee. Lengo lilikuwa kuonesha bidhaa na teknolojia mbalimbali za kilimo, ufugaji na vifungashio vya nafaka. Hii ni njia mojawapo ya kufungua milango ya biashara ili bidhaa zinazozalishwa na watanzania kupata teknolojia nzuri za uzalishaji na hivyo kuwezesha kupata masoko ndani na nje ya nchi na hatimaye kuongeza pato la Taifa
Maonesho haya yalifunguliwa rasmi na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Judith S. Kapinga. Katika ufunguzi huo, Mheshimiwa Waziri alieleza namna serikali inavyozidi kufungua mianya ya biashara ndani na nje ya nchi na kukaribisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali yenye fursa. Waonyeshaji walio wengi ni makampuni kutoka nje ya nchi zikiwemo nchi za India, Israel, Uturuki, Brazil, China na Kenya,
Pia alipata fursa ya kutembelea banda la SIDO na kufurahishwa kwa namba SIDO inavyoshirikiana na wadau mbalimbali katika kusukuma gurudumu la maendeleo nchini. Alielekeza SIDO kuendelea kuwasaidia wajasiriamali na hasa upande wa vifungashio ili bidhaa wanazozalisha ziweze kufungashwa vyema na kupata masoko ya uhakika ndani nan je ya nchi.

