Katika juhudi za kukuza uchumi jumuishi na kuongeza ushindani wa bidhaa za ndani na kimataifa, ENABEL kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) imeendelea kuwawezesha wajasiriamali kwa kuwapatia mafunzo ya kina kuhusu masoko na ufungashaji wa bidhaa.
Mafunzo hayo yalifanywa na Mkufunzi kutoka SIDO Makao Makuu, Bi. Antonia Masoy na yaliyofanyika katika Ofisi za SIDO – Tanga kuanzia tarehe 14 hadi 16 Aprili 2026 na kukutanisha jumla ya wajasiriamali 65, wengi wao wakiwa wanawake. Washiriki walitoka katika sekta mbalimbali zikiwemo uzalishaji wa vyakula, sabuni, vipodozi, na bidhaa za mikono.
Lengo kuu la mafunzo lilikuwa kuwajengea uwezo wajasiriamali katika kuboresha ubora wa bidhaa zao, kuongeza thamani, na kuwasaidia kufikia masoko mapana zaidi ndani na nje ya nchi. Mafunzo haya yalijikita katika maeneo muhimu ya masoko, ujenzi wa chapa (branding), uchaguzi sahihi wa vifungashio pamoja na uwekaji wa lebo zenye viwango vinavyokubalika. Katika eneo la masoko, washiriki walipata uelewa wa kina kuhusu:
- Utafiti wa soko na utambuzi wa wateja lengwa
- Matumizi ya mitandao ya kijamii katika kukuza biashara
- Ujenzi wa chapa (branding) yenye mvuto pamoja na uundaji wa kauli mbiu (taglines)
- Mbinu bora za kuongeza mauzo na kudumisha wateja
Kwa upande wa ufungashaji, mafunzo yalijumuisha:
- Uchaguzi sahihi wa vifungashio kulingana na aina ya bidhaa
- Ubunifu wa lebo zenye mvuto, zenye taarifa muhimu na zinazozingatia matumizi sahihi ya rangi, picha na maandishi (fonts)
- Uzingatiaji wa viwango vya ubora na usalama wa bidhaa
- Umuhimu wa nembo na utambulisho wa bidhaa sokoni
Baadhi ya washiriki walieleza kuwa mafunzo hayo yamewapa mwanga mpya katika namna ya kuboresha bidhaa zao ili ziweze kushindana kikamilifu sokoni. Walibainisha kuwa kabla ya mafunzo hayo, hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mchango mkubwa wa ufungashaji katika kuvutia wateja na kuongeza thamani ya bidhaa.
Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo alisisitiza kuwa maendeleo ya wajasiriamali yanategemea ushirikiano madhubuti kati ya taasisi za umma na sekta binafsi. Ushirikiano kati ya SIDO na ENABEL umetajwa kuwa chachu muhimu katika kukuza uwezo wa wajasiriamali, kuongeza ajira, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Mradi wa ENABEL unaendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za kuwawezesha wajasiriamali nchini, ikiwemo utoaji wa mafunzo, rasilimali, na fursa za mitandao ya kibiashara. Hatua hizi zinawalenga kuwasaidia wajasiriamali kufikia mafanikio endelevu na kuongeza ushindani wa bidhaa za Kitanzania katika masoko ya ndani na ya kimataifa.
Kwa ujumla, mafunzo ya masoko na ufungashaji yameonekana kuwa kichocheo muhimu katika kuboresha biashara za wajasiriamali na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika ushindani wa soko la kisasa.

