WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA AFUNGUA MAONESHO YA SIDO KITAIFA, ATOA WITO MIKOPO KUELEKEZWA KWA WAZALISHAJI
Imewekwa: 28 Oct, 2026
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA AFUNGUA MAONESHO YA SIDO KITAIFA, ATOA WITO MIKOPO KUELEKEZWA KWA WAZALISHAJI

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Judith Kapinga (MB), amefungua rasmi Maonesho ya 5 ya SIDO Kitaifa, yaliyofanyika katika Viwanja vya Magufuli, Kahama – Shinyanga. Maonesho haya yalihudhuriwa na wageni mbalimbali, wakiwemo wakuu wa  taasisi za kiserikali na zile zisizo za kiserikali.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Mheshimiwa Waziri aliipongeza Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) kwa kuratibu maonesho hayo na kueleza kuwa hili ni jukwaa muhimu kwa wajasiriamali kuonesha bidhaa zao, kutangaza biashara zao na kutafuta fursa za kupanua masoko. Aliongeza kuwa kila mjasiriamali ana ndoto ya kukua na kuendeleza biashara yake, hivyo kushiriki katika maonesho haya ni fursa muhimu ya kupanua wigo wa soko la ndani na nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri alieleza kuwa Serikali inatambua mtaji ni kila kitu, hivyo imeweza kutenga kiasi cha shilingi bilioni 14.572 ambacho kitawasaidia wajasiriamali katika uzalishaji. Alitoa wito kuwa mikopo inayotolewa na Serikali iw alenge zaidi wajasiriamali wanaoongeza thamani ya malighafi mbalimbali zinazozalishwa nchini, badala ya kuelekezwa kwa wachuuzi.

Alisema kuwa kuwawezesha wajasiriamali wazalishaji kupata mikopo kutawasaidia kupanua shughuli zao, kuongeza uwezo wa uzalishaji na kuanzisha viwanda mbalimbali vitakavyozalisha bidhaa zenye thamani kubwa zaidi. Hatua hiyo itasaidia kufungua fursa mpya za ajira kwa wananchi, kuongeza kipato na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia shughuli za viwanda. Aidha, alionesha fursa mbalimbali zilizopo na kuziomba taasisi za fedha kushirikiana na SIDO ili kuwezesha zaidi sekta hii ya ujasiriamali.

Amezitaka taasisi zinazotoa huduma kwa wajasiriamali, kama BRELA, TBS na TanTrade, kuhakikisha zinaendelea kutoa huduma zake katika maonesho haya. Alitoa mfano kuwa TBS inaweza kuchukua sampuli za bidhaa zinazooneshwa ili kubaini ubora wake, kwa kuwa maonesho hayo ni sehemu muhimu ya kukutana na bidhaa nyingi za wajasiriamali ambazo hazina alama ya ubora. Pia, ameitaka BRELA kuendelea kutoa elimu kwa wajasiriamali kuhusu faida zilizopo katika kusajili biashara zao. Vilevile, ameitaka TanTrade kuonesha umuhimu wa kuwa na alama ya Made in Tanzania katika bidhaa wanazozalisha na kufungasha.

Maonesho haya yamewakutanisha wajasiriamali kutoka mikoa mbalimbali, ikiwemo washiriki kutoka nchi jirani ya Burundi. Bidhaa mbalimbali zimeoneshwa katika maonesho haya, zikiwemo bidhaa za usindikaji, uhandisi, sabuni na vipodozi, nguo, bidhaa za ngozi na dawa za asili.

Alimalizia kwa kusisitiza umuhimu wa uanzishwaji wa kongani katika kila wilaya, pamoja na kutumia teknolojia za kidijitali zaidi katika kutafuta masoko.

Mwisho, aliwapongeza CRDB Bank Foundation kwa kuwa mfadhili mkuu  wa Maonesho ya 5 ya SIDO Kitaifa ambapo yamefunguliwa rasmi tarehe 24/10/2026.

Matangazo
03 Dec, 2025
23 Nov, 2025
Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo