Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Judith Kapinga (Mbunge), ametembelea Banda la SIDO katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF 2026) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba), jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, Waziri alijionea teknolojia mbalimbali za mashine zinazotumika katika uongezaji thamani mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, pamoja na bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
Akiwa katika banda la SIDO, Waziri alipata fursa ya kuzungumza na wajasiriamali kutoka Tabora na kujionea bidhaa zao ambapo kufurahishwa kuona bidhaa zao zilizokuwa za kiwango na kufanikiwa kupata alama ya ubora kutoka TBS
Aidha, alitembelea mabanda ya vijana wanaojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za urembo, ambao walieleza kufurahishwa na kutembelewa na Waziri pamoja na kupata fursa ya kueleza shughuli zao na mafanikio wanayoyapata kupitia ujasiriamali.
SIDO inaendelea kuwakaribisha wananchi wote kutembelea Banda lake katika Maonesho ya Sabasaba ili kujionea na kununua bidhaa bora zinazozalishwa na wajasiriamali wa Kitanzania. Bidhaa hizo ni pamoja na vyakula vilivyosindikwa, mashine za uzalishaji, bidhaa za ngozi na nguo, sabuni, vipodozi na bidhaa nyingine nyingi zenye ubora wa hali ya juu.

