Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) limeshiriki kikamilifu katika ziara ya kikazi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, mkoani Mtwara iliyofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 13 Novemba 2026. Ziara hiyo ililenga kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo, kukagua utekelezaji wa shughuli za Serikali na kuzungumza na wananchi kuhusu juhudi zinazofanyika kuboresha maisha yao.
Katika ziara hiyo, SIDO ilipata fursa ya kuonesha mchango wake katika kuchochea uanzishwaji, ukuaji na uendelezaji wa viwanda vidogo na vya kati, hususan katika sekta ya uchakataji wa mazao ya kilimo, ambayo ni miongoni mwa sekta zenye fursa kubwa za kiuchumi katika Mkoa wa Mtwara.
Miongoni mwa matukio muhimu katika ziara hiyo ni uzinduzi wa Kongani ya Viwanda Maranje, ambayo inatarajiwa kuwa chachu ya uwekezaji, uzalishaji, uongezaji thamani wa mazao ya kilimo na upatikanaji wa ajira kwa wananchi. Kongani hiyo inalenga kuimarisha mazingira ya uzalishaji na kuvutia wajasiriamali pamoja na wawekezaji kuanzisha na kuendeleza shughuli za viwanda mkoani humo.
Aidha, Mhe. Makamu wa Rais alizindua na kukabidhi jumla ya mashine 100 za ubanguaji korosho kwa wanufaika kupitia uwezeshaji wa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania. Utoaji wa mashine hizo unalenga kuongeza uwezo wa uchakataji wa korosho nchini, kuwawezesha wazalishaji wadogo kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa zao hilo na kuongeza thamani ya korosho kabla ya kuuzwa sokoni.
Katika kuhakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo yaliyokusudiwa, Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia SIDO inaendelea kuwa na nafasi muhimu ya kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu, mafunzo, uendelezaji wa teknolojia na kuwawezesha wajasiriamali kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi viwango na mahitaji ya soko.
Huduma hizo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa uwekezaji unaofanyika katika mashine na vifaa vya uzalishaji unaambatana na matumizi sahihi ya teknolojia, uzalishaji wa bidhaa bora na salama, pamoja na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akishiriki ziara hiyo, Bi. Chresencia Mwimbwa, Mkurugenzi Msaidizi wa Biashara za Nje, Idara ya Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, aliambatana na Meneja wa SIDO Mkoa wa Mtwara, Bi. Merina Mkuchu. Ushiriki wao ulilenga kufuatilia na kuonesha namna taasisi zilizo chini ya Wizara zinavyoweza kushirikiana katika kuwezesha maendeleo ya viwanda na biashara nchini.
Ushiriki wa SIDO katika ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuunganisha uwekezaji unaofanywa na Serikali na huduma za maendeleo ya viwanda zinazotolewa kwa wajasiriamali, ili kuhakikisha kuwa fursa zinazotokana na miradi ya maendeleo zinawafikia wananchi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Mtwara.
Kwa ujumla, ziara hiyo imesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya Serikali, taasisi zake, sekta binafsi na wajasiriamali katika kujenga uchumi unaotegemea uzalishaji, ubunifu na uongezaji thamani wa rasilimali zinazopatikana nchini.
SIDO inaendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kuwezesha ukuaji wa viwanda vidogo na vya kati kupitia huduma za ushauri wa biashara, mafunzo, teknolojia, ubunifu, uendelezaji wa bidhaa na kuwaunganisha wajasiriamali na fursa za masoko na uwekezaji. Juhudi hizi zinalenga kuongeza tija, kukuza ajira, kuimarisha ushindani wa bidhaa za ndani na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.

