SIDO NA CRDB MTWARA YATOA MAFUNZO YA USIMIAMIZI WA FEDHA KWA WAJASIRIAMALI
Imewekwa: 15 May, 2026
SIDO NA CRDB  MTWARA YATOA MAFUNZO YA USIMIAMIZI WA FEDHA KWA WAJASIRIAMALI

Ofisi ya Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na Benki ya CRDB wameendesha mafunzo ya usimamizi wa fedha kwa wajasiriamali wenye shauku ya kupata mikopo kupitia taasisi hizo. Mafunzo hayo yalilenga kuwapa washiriki uelewa wa matumizi sahihi ya mikopo ya biashara pamoja na kuwaonesha fursa mbalimbali za kifedha na aina za mifuko ya mikopo inayopatikana.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Meneja wa SIDO Mkoa wa Mtwara, Bi. Merina Mkuchu, alieleza aina mbalimbali za mikopo inayotolewa kupitia ushirikiano wa SIDO na Benki ya CRDB. Miongoni mwa mifuko aliyoiainisha ni mfuko wa Credit Guarantee Scheme (CGS) unaowezesha wajasiriamali kunufaika na mikopo kupitia Benki ya CRDB kwa udhamini wa SIDO.

Aidha, Bi. Mkuchu alibainisha kuwa SIDO kwa kushirikiana na CRDB Foundation ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuanza kutoa mikopo maalum iliyotengwa na Serikali kwa ajili ya kuwawezesha vijana kukuza shughuli zao za kiuchumi na biashara.

Kwa upande wake, Meneja wa Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Bw. Protas Mwihava, aliwasisitiza wajasiriamali umuhimu wa kuwa na nidhamu ya fedha na kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba benki kama njia ya kukuza mitaji yao na kuimarisha uwezo wa biashara zao. Alieleza kuwa mikopo inapaswa kutumika kwa malengo ya biashara na si kwa matumizi binafsi yasiyohusiana na shughuli za uzalishaji au maendeleo ya biashara.

Mafunzo hayo yalitoa pia nafasi kwa washiriki kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu vigezo vya kupata mikopo, usimamizi wa fedha za biashara pamoja na namna ya kuchagua mfuko wa mkopo unaoendana na mahitaji ya biashara zao.

Kwa mujibu wa waandaaji, zaidi ya mifuko sita ya mikopo imeainishwa kupitia ushirikiano wa SIDO na Benki ya CRDB kwa ajili ya kuwahudumia wajasiriamali wa sekta mbalimbali. Mafunzo hayo yalihitimishwa kwa kuweka mpango wa kutembelea na kutathmini mazingira ya biashara za washiriki ili kubaini aina ya mfuko wa mkopo unaofaa kulingana na mahitaji na uwezo wa biashara husika.

Matangazo
03 Dec, 2025
23 Nov, 2025
Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo