SIDO NA WWF WAIBUA FURSA MPYA ZA KIUCHUMI KWA WAFUGAJI WA NYUKI KOROGWE KUPITIA UTENGENEZAJI WA SABUNI.
Imewekwa: 17 Nov, 2026
SIDO NA WWF WAIBUA FURSA MPYA ZA KIUCHUMI KWA WAFUGAJI WA NYUKI KOROGWE KUPITIA UTENGENEZAJI WA SABUNI.

Katika kuendeleza ubunifu, kuongeza thamani ya mazao ya nyuki na kukuza fursa za kiuchumi zinazozingatia uhifadhi wa mazingira, Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF), limeendesha mafunzo ya utengenezaji wa sabuni kwa kutumia malighafi zitokanazo na asali kwa wanachama wa vikundi vya wakulima na wafugaji wa nyuki katika Wilaya ya Korogwe, Mkoa wa Tanga.

Mafunzo hayo yamewashirikisha wanachama wa vikundi vitatu kutoka vijiji vya Mkumba na Gombero, ambao wamepata ujuzi na maarifa ya namna ya kutumia malighafi zinazotokana na asali kutengeneza bidhaa mbalimbali za sabuni.

Kupitia mafunzo hayo, washiriki wamewezeshwa kutambua fursa zilizopo katika kuongeza thamani ya mazao ya nyuki kwa kuyachakata na kuyabadilisha kuwa bidhaa zenye thamani zaidi sokoni. Hatua hii inatoa fursa ya kupanua wigo wa shughuli za kiuchumi kwa wafugaji wa nyuki, kuongeza vyanzo vya mapato na kupunguza utegemezi wa kuuza asali ghafi pekee.

Aidha, mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuhamasisha ubunifu na matumizi bora ya rasilimali zinazopatikana katika jamii, huku yakichochea uanzishwaji na uendelezaji wa shughuli za uzalishaji zinazoweza kuwa chanzo cha ajira na kipato kwa wananchi.

Ushirikiano kati ya SIDO na WWF unaendelea kuonesha umuhimu wa kuunganisha maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za asili. Kwa kuwajengea wananchi uwezo wa kuongeza thamani ya mazao yao, ushirikiano huo unachangia kujenga jamii zenye uwezo wa kiuchumi huku zikishiriki kikamilifu katika kulinda mazingira.

SIDO na WWF zinaendelea kuhamasisha ubunifu, uongezaji thamani wa mazao na matumizi endelevu ya rasilimali za asili kama mkakati muhimu wa kuimarisha uchumi wa wananchi na kuhakikisha mazingira yanalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Matangazo
03 Dec, 2025
23 Nov, 2025
Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo