SIDO Mkoa wa Njombe inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapatia mafunzo ya ufundi stadi na ujasiriamali. Kupitia mradi wa TFS, vijana wenye ulemavu wanapewa fursa ya kupata mafunzo ya ufundi ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi. Katika utekelezaji wa mpango huu, vijana watano (5) wenye ulemavu tofauti tofauti wanapatiwa mafunzo ya ufundi stadi katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Njombe kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Hivi karibuni, Meneja wa SIDO Mkoa wa Njombe Bi. Neserian Laizer alifanya ziara ya kutembelea na kufuatilia maendeleo ya mafunzo kwa vijana hao watano wanaofadhiliwa na Mradi wa TFS chini ya SIDO - Njombe. Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni:-
- Kufuatilia maendeleo ya mafunzo wanayopata vijana hao
- Kujionea mazingira ya kujifunzia katika chuo hicho
- Kuwatia moyo na kuwahamasisha vijana hao kuendelea na mafunzo yao kwa bidii
Vijana wanaonufaika na mpango huu wanapatiwa mafunzo ya ufundi stadi ambapo wasichana watatu wanapata mafunzi katika fani ya ushonaji na vijana wawili wa kiume wanapata mafunzo katika fani ya useremala.
Kupitia mradi huu, SIDO Njombe imewawezesha vijana hawa kwa kulipia ada za mafunzo pamoja na fedha za matumizi (posho) kwa kipindi chote cha mwaka mmoja, ili kuhakikisha wanapata fursa ya kujifunza bila changamoto za kifedha. Mafunzo haya yanafanyika katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Njombe, ambacho ni chuo cha Serikali kinachotoa mafunzo ya ufundi stadi pamoja na ujasiriamali kwa gharama nafuu.
Mafanikio yanayotarajiwa kupitia mafunzo haya ni pamoja na:
- Kupata ujuzi wa vitendo katika fani walizochagua
- Kujengewa uwezo wa kuanzisha shughuli zao za kiuchumi
- Kupata fursa za kuajiriwa katika sekta mbalimbali za uzalishaji
- Kuongeza ushiriki wa vijana wenye ulemavu katika maendeleo ya kiuchumi
Programu hii ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia SIDO kuhakikisha kuwa vijana wenye ulemavu wanapatiwa fursa sawa za kupata ujuzi na kujitegemea kiuchumi. SIDO Njombe itaendelea kufuatilia maendeleo ya vijana hawa ili kuhakikisha wanapata manufaa stahiki ya mpango huu.

