SIDO Mkoa wa Dar es salaam imepokea ugeni kutoka Shirika lisilo la kiserikali la MO DEWJI FOUNDATION kwa lengo la kuwa ya kujenga mashirikiano ya pamoja. MO DEWJI Foundation imekuwa ikitoa ufadhili chini ya MO SCHOLARSHIP kwa ajili ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo Vikuu. Sambamba na ufadhili huo, MO DEWJI Foundation pia inataka kuanza kutoa ufadhili wa ujuzi wa vitendo kwa vijana katika taasisi zitoazo mafunzo kama SIDO.
Malengo yake ya ufadhili yamejikita katika nyanja kuu tano ambazo ni elimu, afya, msaada wa kijamii, uwezeshaji wa vijana na wanawake na miradi ya maendeleo ya kijamii. Kwa ujumla, MO Foundation hutumia sehemu ya rasilimali zake za biashara kusaidia jamii na kuleta maendeleo kwa kijamii.
Kaimu Meneja wa SIDO Mkoa wa DSM, Bw. Jonathan Mbailuka, alisema kuwa, lengo kuu la ujio huo umetokana na andiko la Mradi lililowasilishwa na Ofisi ya Mkoa juu ya kuomba mashirikiano katika kutoa mafunzo ya uwezeshaji vijana kiuchumi hasa vijana waliohitimu katika vyuo mbalimbali. Hii itawawezesha kujiunga na mafunzo yanayotolewa na SIDO yakiwemo uchakataji wa vyakula; uongezaji thamani bidhaa za ngozi; utengenezaji vifaa vya elektroniki kama simu; utengenezaji wa batiki; usindikaji wa maziw; uchomeleaji na fani nyinginezo.
Mmoja wa wakilishi kutoka MO DEWJI FOUNDATION, Bwana Samson, alisema kuwa wapo tayari kushirikiana na SIDO katika masuala mbalimbali ikiwemo ufadhili wa mafunzo ya ujuzi na kutoa uwezeshaji kwa vijana na wanawake katika kuanzisha miradi ya kiuchumi.
Pande zote mbili zilikubaliana kukutana na Mkurugenzi Mtendaji, Bw. MO DEWJI katika kipindi cha muda mfupi ujao kwa ajili ya kupitia kwa pamoja andiko la Mradi la kuwezesha na kuwafadhili Vijana. Pia taasisi ya MO DEWJI FOUNDATION imesema iko tayari kutoa ufadhili kupitia MO SCHOLARSHIP na mitaji midogo midogo kwa vijana watakaohitimu mafunzo ya ujuzi kupitia SIDO.

