Dawati Maalumu la Uwezeshaji Biashara Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na SIDO limetoa mafunzo ya elimu ya kodi na uwezeshaji wa biashara kwa wajasiriamali na wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali. Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara pamoja na uelewa wa masuala ya kodi ili kukuza biashara zao kwa kuzingatia taratibu za kisheria.
Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Meneja Msaidizi wa Huduma kwa Walipa Kodi, Bw. Mohamed Kapera, aliwahimiza wafanyabiashara kujisajili na kurasimisha biashara zao ili kunufaika na fursa mbalimbali za Serikali. Pia aliwashauri ambao bado hawana Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kujisajili ili kutambulika rasmi katika mfumo wa kodi.
Katika mafunzo hayo, Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi kutoka TRA, Bw. Isaka Mwangoi, alitoa elimu kuhusu mambo muhimu kwa mtu anayeanza biashara ikiwemo kupata TIN, kufanya makadirio sahihi ya mapato na kufuata taratibu za kodi. Mafunzo hayo pia yalihusisha usajili wa TIN mpya kwa baadhi ya washiriki.
Aidha, Maafisa wa Kodi Bi. Agripina Malya na Bi. Haika Malya walishiriki kutoa msaada kwa washiriki pamoja na kusajili Namba za Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa wajasiriamali waliohitaji huduma hiyo wakati wa mafunzo. Naye Mratibu wa Miradi na Mafunzo kutoka SIDO, Bw. Stephano Nduguru, aliishukuru TRA kwa kutoa elimu ya kodi kwa wajasiriamali na wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali. Kwa upande wake, Afisa wa Dawati Maalumu la Uwezeshaji Biashara, Bi. Sauda Sangisha, alisema dawati hilo linaendelea kutoa elimu na ushauri kwa wafanyabiashara ili kuwajengea uwezo na kuwahamasisha kurasimisha biashara zao, hatua inayosaidia kupanua wigo wa kodi.

