Vijana 21 wamepatiwa mafunzo ya siku 14 kuhusu matumizi sahihi ya vyerehani pamoja na kufanya matengenezo madogo ya mashine walizopata kupitia Mradi wa TFS. Mafunzo hayo yamelenga kuwaongezea ujuzi wa kutumia na kutunza vifaa vyao kwa usahihi, pamoja na kutambua na kurekebisha hitilafu ndogo za vyerehani.
Aidha, vijana hao wameelimishwa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na SIDO na namna wanavyoweza kuzitumia katika kuendeleza shughuli zao za uzalishaji na biashara.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwawezesha vijana kupunguza gharama za matengenezo, kupunguza muda wa kusimamisha uzalishaji na kuongeza ufanisi na tija katika shughuli zao za ushonaji. Ujuzi walioupata pia utawasaidia kuongeza uzalishaji na kipato, kuimarisha biashara zao, kujiajiri na hatimaye kuunda fursa za ajira kwa vijana wengine.
SIDO itaendelea kuwafuatilia na kuwapatia ushauri wa kitaalamu ili kuhakikisha vyerehani vilivyotolewa vinatumika na kutunzwa ipasavyo, na kwamba vijana hao wanatumia ujuzi walioupata kujenga biashara endelevu na zenye tija.

