Zao la kakao (Cocoa ) ni zao la biashara lenye soko zuri kimataifa, lakini bado halijakua sana ukilinganisha na mazao mengine kama vile kahawa au korosho. Mahitaji ya dunia yanaongezeka hivyo linaweza kuwa zao lenye faid kubwa kama litwekewa uwekezaji. Nchini Tanzania, Kakao hustawi katika maeneo ya mikoa ya nyanda za juu Mbeya, Songwe, Njombe , Songea na Ruvuma kutokana na hali ya ya hewa ya joto kiasi na mvua nyingi.
Kakao ya Kyela ni miongoni mwa kakao bora inayolimwa pasipo kutumia mbolea (organic) na limekuwa zao la kimkakati na hutumiwa katika tasnia ya dawa,vyakula na vipodozi n.k. Zao hili limeleta fursa za ajira kwa vijana na wanawake pamoja na utunzaji wa mazingira kutokana na mti wa kakao kutengeneza kivuli kizuri. Wakulima wa kakao wanakabiliwa na changamoto ya ukaushaji kipindi cha mvua na ujuzi wa kuchakata kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbalimbali.
SIDO ilipata nafasi ya kutembelea Chama kikuu cha Ushirika Kyela (KYECU) ili kujionea namna chama hicho kinavyowasaidia wakulima wa kakao wilayani Kyela. Pamoja na mambo mengi waliyojadili, Meneja wa SIDO - Mbeya Bi. Salma Galasi akiongozana na wafanyakazi wengine, waliona ipo haja ya kuwasaidia wakulima wa zao hili kupata makaushio ya kisasa yatakayorahisisha uanikaji wa kakao wakati wa msimu wa mvua ili kuweza kupata kakao iliyo bora. Pia kulionekana upo uhitaji wa mashine za kuchakata kakao na hii itasaidia kuongeza mnyororo wa thamani wa zao la kakao, uanzishaji wa viwanda vipya na kuongeza ajira kwa vijana. KYECU kinasimamia jumla ya vyama vya msingi 37 ( Amcos) na idadi kuu ya wanachama ni 3700.

