Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Morogoro limeshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Cocoa Tanzania yaliyofanyika Wilaya ya Mlimba. Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na kuratibiwa na Wilaya ya Kilombero yalilenga kuhamasisha uzalishaji, uongezaji thamani pamoja na masoko ya zao la cocoa nchini.
Wilaya ya Mlimba ni ya pili kwa uzalishaji wa zao la cocoa nchini Tanzania, ambapo takribani tani 200 za cocoa huuzwa kila mwaka, jambo linaloonesha mchango mkubwa wa zao hilo katika kukuza uchumi wa wananchi wa eneo hilo.
Katika maadhimisho hayo, SIDO Morogoro ilipata fursa ya kutoa elimu kwa wakulima, wajasiriamali na wadau mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuongeza thamani ya mazao kupitia usindikaji wa bidhaa za cocoa, matumizi ya vifungashio bora pamoja na mbinu za kuongeza ushindani wa bidhaa katika soko la ndani na nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo, mwakilishi wa SIDO Morogoro, Bi. Marietha Kalolo, alieleza kuwa Shirika linaendelea kuwawezesha wajasiriamali kupitia mafunzo ya biashara, teknolojia za mashine za usindikaji, ubunifu wa bidhaa pamoja na kuwaunganisha na fursa za masoko ili kuongeza kipato na ajira kwa wananchi.
Aidha, wananchi waliotembelea banda la SIDO walipata nafasi ya kujionea bidhaa mbalimbali zinazotokana na cocoa pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu namna ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za uongezaji thamani wa mazao ya kilimo.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa changamoto kubwa inayowakabili wazalishaji wa cocoa ni upatikanaji wa pembejeo pamoja na mashine za kisasa zenye uwezo wa kusaidia wakulima kuongeza thamani ya mazao yao na kuzalisha bidhaa mbalimbali kama cocoa powder, chocolate na cocoa syrup.
Maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa sekta ya cocoa, kubadilishana uzoefu na kujadili mikakati ya kuendeleza zao hilo kwa maendeleo ya uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

