NJOMBE YAFANYA KIKAO NA WAWAKILISHI WA SHIRIKA LA COMPASSION KUJADILI MAENEO YA USHIRIKIANO
Imewekwa: 08 Sep, 2026
NJOMBE YAFANYA KIKAO NA WAWAKILISHI WA SHIRIKA LA COMPASSION KUJADILI MAENEO YA USHIRIKIANO

Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Njombe limefanya kikao na wawakilishi 14 wa Shirika la Compassion, wakiongozwa na Mratibu wa Kanda ya Kusini, Bw. Felician Tillya, inayojumuisha mikoa ya Njombe, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Katika kikao hicho, Meneja wa SIDO Njombe aliwasilisha na kuelezea huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika, pamoja na kujadiliana na wawakilishi hao kuhusu maeneo ya uwezekano wa ushirikiano katika kuwawezesha wajasiriamali na walengwa wa Compassion.

Maeneo yaliyobainishwa kwa ajili ya ushirikiano ni pamoja na mafunzo ya ujasiriamali, huduma za ushauri (Advisory Services) na teknolojia, hususan teknolojia zinazolenga kuongeza ufanisi na tija katika shughuli za uongezaji thamani wa malighafi mbalimbali zinazozalishwa hapa nchini.

Ushirikiano huo unalenga kuwajengea uwezo walengwa wa Compassion kwa kuwapatia maarifa, ujuzi na huduma zinazohitajika ili kuanzisha, kuendeleza na kukuza shughuli zao za kiuchumi, pamoja na kuwaunganisha na huduma na fursa mbalimbali zinazotolewa na SIDO.

Hatua inayofuata ni kuendelea na majadiliano kati ya SIDO na Compassion ili kuweka utaratibu madhubuti wa utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano yaliyobainishwa.

Ushirikiano huu unatarajiwa kutoa fursa zaidi kwa walengwa wa Compassion kupata huduma za kitaalamu na teknolojia zinazotolewa na SIDO, huku ukiimarisha juhudi za pamoja katika kuwawezesha wajasiriamali na kuongeza fursa za kiuchumi katika Kanda ya Kusini.

SIDO – PAMOJA TUJENGE VIWANDA

Matangazo
03 Dec, 2025
23 Nov, 2025
Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo