SIDO NJOMBE YATUMIA TEKNOLOJIA KUWAJENGEA UWEZO VIJANA WA MAKETE KATIKA UZALISHAJI WA KOKOTO
Imewekwa: 16 Nov, 2026
SIDO NJOMBE YATUMIA TEKNOLOJIA KUWAJENGEA UWEZO VIJANA WA MAKETE KATIKA UZALISHAJI WA KOKOTO

Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Mkoa wa Njombe, limeendelea kutekeleza juhudi za kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapatia mafunzo ya kiufundi na ujasiriamali vijana wanane wa Kikundi cha Vijana Makete cha Kuchakata Kokoto na Mawe, wilayani Makete, Mkoa wa Njombe.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 7 Novemba 2026, yalilenga kuwajengea vijana hao uwezo wa kutumia teknolojia katika uchakataji wa mawe na uzalishaji wa kokoto, pamoja na kuwaongezea ujuzi wa kusimamia shughuli zao za uzalishaji na biashara.

Kupitia wataalamu wake, SIDO iliwawezesha vijana hao kupata ujuzi wa vitendo kuhusu uendeshaji na matumizi sahihi ya mtambo wa kusaga mawe na kuzalisha kokoto (Crusher). Aidha, walijifunza namna ya kufanya matengenezo ya kawaida ya mtambo ili kuhakikisha unafanya kazi kwa ufanisi, kuongeza tija na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa uzalishaji.

Mbali na mafunzo ya kiufundi, vijana hao pia walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali yaliyohusisha utunzaji wa kumbukumbu za biashara, usimamizi wa fedha na uelewa kuhusu fursa za mikopo zinazoweza kuwasaidia kuendeleza na kupanua shughuli zao za uzalishaji.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwawezesha vijana kuongeza ujuzi na ufanisi katika uzalishaji, kuimarisha usimamizi wa biashara zao, kujiajiri na kuongeza kipato. Vilevile, uwezeshaji huo unalenga kuchochea shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Wilaya ya Makete na Mkoa wa Njombe kwa ujumla.

Kupitia mafunzo hayo, SIDO inaendelea kusisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo, kukuza ujasiriamali na kuimarisha ushiriki wa vijana katika shughuli za uzalishaji mali.

SIDO Mkoa wa Njombe inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kukuza na kuendeleza viwanda vidogo kupitia utoaji wa teknolojia, mafunzo ya ujuzi, ushauri wa kitaalamu na huduma za maendeleo ya biashara, kwa lengo la kuwawezesha wajasiriamali kuongeza tija, kujenga ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa

 

Matangazo
03 Dec, 2025
23 Nov, 2025
Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo