Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Mkoa wa Njombe, limetoa mafunzo ya uokaji wa bidhaa mbalimbali zitokanazo na unga wa ngano kwa wajasiriamali wa Kikundi cha MAPEMBELO wilayani Makete, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwaongezea ujuzi wa uzalishaji na kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 13 Novemba 2026 yalijikita katika kuwajengea washiriki ujuzi wa kinadharia na vitendo kuhusu utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za mikate na vitafunwa. Bidhaa walizofundishwa kuandaa ni pamoja na mikate, maandazi, keki za aina mbalimbali, upambaji wa keki, biskuti (biscuits), kuki (cookies) pamoja na bidhaa nyingine zinazotokana na unga wa ngano.
Kupitia mafunzo hayo, wajasiriamali walipata fursa ya kujifunza na kufanya mazoezi ya moja kwa moja ya hatua mbalimbali za uzalishaji, kwa lengo la kuongeza ufanisi, kuboresha ubora wa bidhaa na kuimarisha uwezo wao wa kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko.
Lengo kuu la mafunzo hayo lilikuwa kuwawezesha wajasiriamali kuongeza ujuzi na ubunifu katika uzalishaji, kuongeza thamani ya bidhaa, kupanua wigo wa shughuli za biashara na kujenga uwezo wa kujiajiri pamoja na kuongeza kipato.
Akihitimisha mafunzo hayo rasmi siku ya Ijumaa, tarehe 13 Novemba 2026, Bi. Jacklina Thomas Mrosso, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Makete, alishiriki katika kufunga mafunzo hayo yaliyolenga kuwawezesha wajasiriamali kutumia ujuzi walioupata katika kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
SIDO Mkoa wa Njombe inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuwawezesha wajasiriamali na kukuza viwanda vidogo kupitia utoaji wa mafunzo ya ujuzi, uhamishaji wa teknolojia, ushauri wa kitaalamu na huduma nyingine za maendeleo ya biashara.
Jitihada hizi zinalenga kuongeza tija katika uzalishaji, kuboresha ubora na ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini, kukuza fursa za ajira na kuongeza kipato cha wajasiriamali, hivyo kuchangia maendeleo ya uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

