Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO) Mkoa wa Njombe limetembelea kiwanda kidogo cha usindikaji wa unga lishe pamoja na viungo kinachojulikana kama RICHRAY INVESTMENT kilichopo katika eneo la SIDO, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuimarisha maendeleo ya viwanda vidogo na kuongeza thamani ya mazao ya ndani.
Katika ziara hiyo, wataalamu wa SIDO walipata fursa ya kukagua shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazofanyika katika kiwanda hicho pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa mjasiriamali kuhusu namna bora ya kuboresha shughuli za uzalishaji ili kuongeza ufanisi wa biashara na ushindani wa bidhaa sokoni.
Miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na mpangilio bora wa kiwanda, uboreshaji wa mazingira ya uzalishaji, udhibiti wa ubora wa bidhaa, matumizi ya vifungashio vinavyokidhi viwango pamoja na kuzingatia taratibu muhimu za usajili na uthibitishaji wa bidhaa kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
SIDO ilieleza kuwa kufuata viwango vya ubora ni hatua muhimu kwa wajasiriamali wanaolenga kupanua masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi, kwani huongeza imani kwa walaji na kuimarisha ushindani wa bidhaa katika soko.
Kwa upande wake, mmiliki wa RICHRAY INVESTMENT alieleza kufurahishwa na ziara hiyo pamoja na ushauri alioupata, akisema utasaidia kuboresha shughuli za uzalishaji na kuongeza ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada endelevu za SIDO za kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo na kuwawezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la kisasa.

