SIDO YAIBUA MAFANIKIO KATIKA KUWAWEZESHA WAJASIRIAMALI NA KUKUZA VIWANDA
Imewekwa: 28 Oct, 2026
SIDO YAIBUA MAFANIKIO KATIKA KUWAWEZESHA WAJASIRIAMALI NA KUKUZA VIWANDA

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), CPA Ahmed Kitara, amewahimiza wananchi na wajasiriamali kufuatilia kwa karibu fursa mbalimbali za mikopo na huduma nyingine zinazotolewa na SIDO. Hatua hii inalenga kukuza biashara, kuongeza uzalishaji, na hatimaye  kutengeneza ajira.

Akizungumza wakati wa  hotuba ya ufunguzi wa Maonesho yanayoendelea katika Viwanja vya Magufuli mjini Kahama, Kaimu Mkurugenzi alibainisha kuwa maonesho hayo yanalenga kuwawezesha wajasiriamali, kuongeza tija na kupanua masoko ya bidhaa zao. Alieleza kuwa maonesho hayo ni jukwaa mwafaka linalowakutanisha wajasiriamali, wamiliki wa viwanda, taasisi za fedha, watoa huduma za teknolojia na wanunuzi.  Hii inawapa fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu, na kujenga mahusiano imara ya kibiashara.

Aidha alifafanua kuwa  huduma zinazotolewa na SIDO zimeleta mafanikio makubwa katika kuanzisha viwanda vipya na kuongeza ajira za kudumu nchini. Alitoa mfano wa miaka mitatu ya fedha (kuanzia mwaka 2023/2024 hadi 2025/2026), ambapo jumla viwanda vipya 1,760 vilianzishwa na ajira mpya za kudumu 60,777 zikitengenezwa.

Zaidi ya hayo, katika kipindi hicho hicho, wajasiriamali 51,799 walipewa mafunzo mbalimbali, huku wajasiriamali wengine 71,165 wakinufaika na huduma za ushauri wa kitaalamu na kibiashara.

Kuhusu uwezeshaji wa mitaji, Kaimu Mkurugenzi alisema kuwa jumla ya mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 14.57 ilitolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Ujasiriamali wa Taifa (NEDF), na kuchangia upatikanaji wa ajira 13,482. Aliongeza kuwa SIDO ina mifuko mbalimbali inayolenga kuwawezesha wajasiriamali kupata mitaji, ikiwemo NEDF, CGS na SANVN. Vilevile, SIDO ina mashirikiano na benki mbalimbali ikiwemo CRDB katika uwezeshaji vijana kiuchumi.

Katika hatua nyingine, alieleza kuwa mashine 1,879 zilizalishwa, huku wajasiriamali 4,514 wakisaidiwa kushiriki katika maonesho ya kikanda na kitaifa kwa lengo la kutangaza bidhaa zao na kupanua fursa za masoko.

Kaimu Mkurugenzi alisisitiza kuwa maonesho hayo yanatoa fursa muhimu kwa wananchi kujionea  juhudi za Serikali katika kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa ndani zinakidhi viwango vya ubora na kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Alisema kuwa SIDO itaendelea kuboresha huduma zake na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali. Leng oni kuhakikisha wajasiriamali wengi zaidi  wananufaika na fursa za mafunzo, ushauri wa kitaalamu, teknolojia, mitaji, Pamoja na upatikanaji wa masoko.

Akihitimisha hotuba yake, Kaimu Mkurugenzi aliwashukuru viongozi, wajasiriamali na wadau wote walioshiriki katika maonesho hayo, huku akiwatakia mafanikio mema katika shughuli zao.

 

Matangazo
03 Dec, 2025
23 Nov, 2025
Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo