Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inasisitiza umuhimu wa kila mwananchi, kaya na taasisi za umma na binafsi kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira, kurejesha uoto wa asili na kuhifadhi vyanzo vya maji kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Katika kuunga mkono azma hiyo, Manispaa ya Shinyanga ilizindua rasmi kampeni ya upandaji miti kwa msimu wa mvua wa mwaka 2026/2027 tarehe 20 Novemba 2026, katika eneo la Zahanati ya Ibinzamata, kwa lengo la kupanda miti milioni 1.5 ndani ya Manispaa ya Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya lengo la kupanda jumla ya miti milioni 3 katika Wilaya nzima ya Shinyanga. Katika siku ya uzinduzi, jumla ya miti 1,500 ilipandwa. Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga.
Ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kushiriki katika shughuli za maendeleo ya taifa na kuimarisha utunzaji wa mazingira, Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Mkoa wa Shinyanga, liliungana na wadau wengine kushiriki katika kampeni hiyo kwa kupanda miti katika eneo la Ibinzamata, ikiwa ni mchango wake katika kufanikisha azma ya kuifanya Shinyanga kuwa ya kijani na endelevu kimazingira.
Katika kampeni hiyo, viongozi na wadau mbalimbali walihimiza jamii kupunguza ukataji holela wa miti unaochochewa na matumizi ya kuni na mkaa kama nishati ya kupikia, na badala yake kuhamasisha matumizi ya nishati safi na mbadala ili kulinda misitu na kuhifadhi mazingira.
Kwa upande wake, SIDO ni mdau muhimu katika juhudi za kupunguza ukataji miti kupitia uendelezaji na usambazaji wa teknolojia za nishati safi na mbadala. Miongoni mwa teknolojia hizo ni utengenezaji wa mkaa mbadala (briquettes) kwa kutumia mabaki ya mazao ya kilimo kama maganda ya mpunga, vifuu vya nazi na mabaki mengine ya mimea. Teknolojia hii husaidia kutumia rasilimali zilizopo kwa tija na kupunguza utegemezi wa mkaa unaotokana na ukataji wa miti.
Aidha, SIDO hutoa mafunzo kwa wajasiriamali na kuwawezesha kuanzisha viwanda vidogo vya kutengeneza majiko banifu yanayotumia nishati kidogo, hivyo kupunguza matumizi ya kuni na mkaa. Kupitia vituo vyake vya teknolojia, Shirika pia hubuni na kutengeneza mashine za kuchakata malighafi na kuzalisha nishati mbadala kulingana na mahitaji ya wajasiriamali.
Ushiriki wa SIDO katika kampeni hii unaonesha dhamira ya Shirika ya kuunganisha maendeleo ya viwanda vidogo na ulinzi wa mazingira kupitia matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, ubunifu na ujasiriamali wa kijani.
Zoezi hilo lililofanyika chini ya kaulimbiu “Shinyanga ya Kijani, Mtu na Mti” lilihusisha wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za umma na binafsi, shule pamoja na wananchi, likilenga kujenga mwamko wa pamoja kuhusu umuhimu wa upandaji miti, uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.
Kupitia ushiriki wake na teknolojia anazozikuza, SIDO inaendelea kuchangia katika utekelezaji wa vipaumbele vya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, hususan maendeleo endelevu yanayozingatia uhifadhi wa mazingira, matumizi bora ya rasilimali na ukuaji wa viwanda unaozingatia ustawi wa jamii na vizazi vijavyo.

