Kikundi cha Danduu Safi kutoka mkoani Shinyanga kimefanikiwa kujikwamua kiuchumi kupitia mafunzo ya vitendo ya utengenezaji wa sabuni za miche na sabuni za kuogea yaliyotolewa na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Mkoa wa Shinyanga.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea wanakikundi uwezo wa kujiajiri na kuendesha shughuli za uzalishaji kwa tija, kwa kuwapatia ujuzi katika utambuzi na uchanganuzi wa malighafi, matumizi ya mbinu bora na za kisasa za uzalishaji, pamoja na usimamizi wa masoko.
Aidha, kupitia mafunzo hayo, wanakikundi wamepata uelewa wa namna ya kuandaa Mpango wa Biashara wa kikundi utakaowawezesha kupanga na kusimamia shughuli zao za kiuzalishaji na kibiashara. Vilevile, wamepatiwa elimu kuhusu taratibu na mahitaji ya kupata alama ya ubora ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hatua muhimu katika kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi viwango vya ubora na kuwa na ushindani sokoni.
Kikundi cha Danduu Safi kilianzisha shughuli za utengenezaji wa sabuni baada ya kubaini kuwa kuna uhitaji mkubwa wa bidhaa hizo katika eneo lao. Uamuzi huo umekuwa fursa ya kujenga chanzo cha mapato kupitia uzalishaji wa bidhaa zinazohitajika katika matumizi ya kila siku ya jamii.
Kwa sasa, kikundi hicho kina jumla ya wanachama 18, wanawake na wanaume, ambao wanaendelea kushiriki katika shughuli za uzalishaji. Kupitia ujuzi walioupata, kikundi kimeweza kuongeza fursa za kipato na kuimarisha mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wanachama.
Katika hatua nyingine, kikundi hicho kipo katika mchakato wa kuomba mkopo utakaowawezesha kununua mashine za kisasa za uzalishaji, ili kuongeza ufanisi, kupanua uwezo wa uzalishaji na kukidhi mahitaji ya soko yanayoongezeka.
Mafanikio ya Kikundi cha Danduu Safi yanaonesha umuhimu wa mafunzo ya vitendo katika kuwawezesha wananchi kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao kujiajiri na kuanzisha shughuli za kiuchumi zenye tija.
Kupitia programu zake za mafunzo, ushauri wa kitaalamu na kuwaunganisha wajasiriamali na fursa za mitaji na masoko, SIDO inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kukuza ujasiriamali, kuendeleza viwanda vidogo na vya kati, kuongeza ajira na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii.

