Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Trade Development Authority (TANTRADE), Bw. Ephraim Mafuru, ametembelea kiwanda cha AKROS Cashew Factory kilichopo katika eneo la SIDO Mtwara, ikiwa ni sehemu ya ziara za Serikali za kutambua na kuendeleza fursa za biashara, viwanda na uongezaji thamani wa mazao ya ndani.
Akiwa kiwandani, Bw. Mafuru aliambatana na Meneja wa SIDO Mkoa wa Mtwara, Bi. Merina Mkuchu, na kupokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa AKROS, Bw. John Joseph Nkundwanabake. Alijionea shughuli za uchakataji wa korosho na kujadiliana na uongozi wa kiwanda kuhusu namna ya kuongeza ubora, thamani na ushindani wa bidhaa za korosho katika masoko ya ndani na nje ya Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE alisisitiza umuhimu wa kuboresha lebo za bidhaa kwa kuzingatia taarifa muhimu zinazohitajika sokoni, pamoja na kupata alama ya “Made in Tanzania” ili kuimarisha utambulisho na uaminifu wa bidhaa za AKROS.
Ziara hiyo pia imeonesha mchango wa SIDO Mtwara katika kuwawezesha wajasiriamali, ikiwemo kutoa eneo la uzalishaji na kuwaunganisha na fursa za masoko na wadau wa biashara.
Ushirikiano kati ya SIDO, TANTRADE na sekta binafsi ni muhimu katika kuongeza thamani ya korosho, kukuza viwanda, kuongeza ajira na kufungua masoko mapya ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

