Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (Warehouse Receipts Regulatory Board – WRRB), chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, Ndug. Asangye Bangu, ametembelea Ofisi ya Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Mtwara, ambapo amefanya mazungumzo na Meneja wa SIDO Mkoa wa Mtwara, Bi. Merina Mkuchu, kuhusu uwezekano wa kuimarisha ushirikiano wa taasisi hizo katika kuendeleza teknolojia za kuboresha ubora wa mazao yanayowasilishwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
Katika mazungumzo hayo, WRRB imeainisha umuhimu wa kutumia utaalamu na uwezo wa kiteknolojia wa SIDO katika kubuni na kuendeleza suluhisho bunifu litakalosaidia AMCOS kudhibiti na kuhakiki ubora wa mazao kabla na wakati wa kuwasilishwa kwenye maghala yanayotumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
Teknolojia hiyo inalenga, miongoni mwa mambo mengine, kuwezesha utambuzi wa uchafu, visivyokidhi viwango na changamoto nyingine zinazoathiri ubora wa mazao, ili kuhakikisha mazao yanayowasilishwa na kuhifadhiwa maghalani yanakuwa safi, salama na yenye ubora unaokubalika kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa.
Kwa upande wake, Meneja wa SIDO Mkoa wa Mtwara, Bi. Merina Mkuchu, ameahidi kulifanyia kazi suala hilo kwa kushirikiana na WRRB pamoja na viongozi wa AMCOS katika Mkoa wa Mtwara. Ushirikiano huo utalenga kukusanya taarifa na kubaini mahitaji halisi ya wadau ili kuwezesha SIDO kubuni teknolojia inayolenga kutatua changamoto hiyo kwa ufanisi na kuendana na mazingira halisi ya uzalishaji na uhifadhi wa mazao.
Ushirikiano huu unaonesha umuhimu wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kutumia kwa pamoja utaalamu, rasilimali na uwezo wa kiteknolojia katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wazalishaji na wadau katika minyororo ya thamani.
Kwa WRRB na SIDO, ushirikiano huo unalenga kuunganisha udhibiti wa ubora wa mazao, ubunifu na teknolojia, kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao, kulinda maslahi ya wakulima, kupunguza upotevu na changamoto za ubora, na hatimaye kuimarisha ufanisi na ushindani wa biashara ya mazao kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

