WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA, AITEMBELEA SIDO
Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (MB) alitembelea Ofisi za Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) zilizopo Upanga Dar Es Salaam kwa lengo la kupata uelewa wa shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika katika kukuza sekta ya Viwanda nchini. kujionea utendaji na utekelezaji wa majukumu ya Shirika. Akipokelewa na mwenyeji wake Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Mhand. Prof. Sylvester Mpanduji, wajumbe wa bodi na watumishi wa SIDO, Waziri aliweza kupatiwa taarifa fupi kuhusu namna Shirika linavyokuza sekta ya viwanda nchini. Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya SIDO, Prof. Musa Nyamsegwa aliongeza kuwa Shirika linatambua mwamko mkubwa wa wananchi katika kuanzisha na kuendelezaji Viwanda Vidogo. Aliahidi kuwa, SIDO itaendelea kuboresha huduma zake, kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi na kuhakikisha wananchi wanazifikia huduma hizo kwa urahisi. Katika hotuba yake, Waziri aliipongeza SIDO na kuahidi ushirikiano katika kuongeza ajira kwa vijana nchini. Alitoa maelekezo kwa Bodi na Menejimenti ya SIDO kuhusu kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika kujenga uchumi wa viwanda na utengenezaji zaidi wa ajira kwa vijana nchini. Pia aliwataka watumishi wa SIDO kutekeleza mipango kazi yenye tija ili kuchochea ajira nyingi nchini kupitia viwanda vidogo, hususan kwa kundi maalumu la vijana. Waziri alisema maagizo hayo yanaenda sambamba na dira ya taifa ya 2050, iliyozinduliwa julai 17 ambayo miongoni mwa malengo yake ni kutoa ajira kwa watanzania ifikapo mwaka 2030. Alisisitiza kuwa jukumu la SIDO ni muhimu katika kufanikisha azma hiyo kwa kuhakikisha miradi na mikakati wanayoipanga inalenga matokeo halisi kwa wananchi. Aidha, waziri Kapinga amewataka watumishi wa SIDO kuunga mkono jitihada na ahadi za Rais ndani ya siku 100, ikiwemo utekelezaji wa Mfuko wa Fedha wa Sh Bilioni 200 pamoja na uanzishwaji wa mitaa ya viwanda katika kila wilaya nchini. Alisema hatua hizo zitatoa fursa pana zaidi za ajira kuinua uchumi wa wananchi, hasa vijana. Nae, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Serera, alisema SIDO ni injini muhimu ya kukuza sekta ya Viwanda Vidogo na kuongeza mchango wake kwenye uchumi wa Taifa. Amesisitiza kuwa Wizara itaendelea kuunga mkono juhudi za Shirika katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo