img
SIDO MTWARA YATOA MAFUNZO YA UONGEZAJI THAMANI ZAO LA MWANI KWA WAJASIRIAMALI WA NAUMBU Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) mkoa wa Mtwara imetoa mafunzo ya siku moja kwa wajasiriamali wanaojishughulisha na shughuli za uongezaji thamani wa zao la mwani katika Kata ya Naumbu, iliyopo Wilaya ya Mtwara Vijijini. Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wajasiriamali katika kuboresha bidhaa zao ili ziweze kukidhi mahitaji ya soko la ushindani kupitia matumizi ya vifungashio vyenye ubora, uwekaji sahihi wa lebo, matumizi ya majina ya biashara pamoja na majina ya bidhaa yanayovutia na kutambulika kirahisi sokoni. Katika mafunzo hayo, washiriki walipata elimu kuhusu umuhimu wa kuongeza thamani ya zao la mwani kwa kuzingatia ubora wa bidhaa, muonekano wa kifungashio na mbinu bora za masoko ambazo zinaweza kuongeza thamani ya bidhaa na kuwasaidia kupata masoko mapana zaidi. SIDO imeeleza kuwa itaendelea kutoa ushauri na huduma mbalimbali kwa wajasiriamali hao, ikiwemo huduma za teknolojia, mafunzo ya ujasiriamali, ushauri wa kifedha pamoja na kuwaunganisha na fursa za masoko ili kuwezesha uzalishaji wa bidhaa zinazoweza kushindana katika soko na kuongeza kipato pamoja na ajira kwa wananchi wa Kata ya Naumbu na maeneo jirani. Jumla ya wajasiriamali 74 walishiriki katika mafunzo hayo, ambapo wanawake walikuwa 66 na wanaume 8. Aidha, kati ya washiriki hao vijana walikuwa 28 huku watu wazima wakiwa 46. Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia SIDO za kuendelea kuwawezesha wajasiriamali wadogo kuongeza thamani ya mazao ya ndani na kuchangia maendeleo ya uchumi wa wananchi.
Matangazo
03 Dec, 2025
23 Nov, 2025
Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo