img
SIDO YAJENGEWA UWEZO KUWAWEZESHA WAJASIRIAMALI KUPATA FEDHA ZA KUENDELEZA BIASHARA Wataalam wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) kutoka mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma na Singida wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo katika uandaaji wa mipango ya biashara na usimamizi wa fedha, hatua inayolenga kuimarisha huduma zinazotolewa kwa wajasiriamali wadogo nchini. Mafunzo hayo yaliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika Jiji la Arusha yamelenga kuwawezesha wataalam hao kutoa ushauri na huduma bora kwa wajasiriamali, hususan katika uandaaji wa mipango ya biashara pamoja na maandiko yenye ubora kwa ajili ya kuomba mikopo na mitaji kutoka taasisi mbalimbali za kifedha. Kupitia mafunzo hayo, wataalam wa SIDO wamepata uelewa na ujuzi unaotarajiwa kuwawezesha kuwasaidia wajasiriamali kuandaa mipango ya biashara inayozingatia mahitaji ya taasisi za kifedha, pamoja na kuimarisha uwezo wao katika usimamizi wa fedha za biashara. Mafunzo hayo pia yamewashirikisha wataalam kutoka Idara za Maendeleo ya Jamii, Idara za Biashara za Mikoa na Halmashauri, pamoja na VETA, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wajasiriamali. Aidha, mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza uwezo wa wajasiriamali katika kupata mitaji kupitia taasisi za fedha, jambo litakalochangia ukuaji wa biashara, uzalishaji na ajira, pamoja na kuongeza mchango wa sekta ya viwanda vidogo katika maendeleo ya uchumi wa Taifa. SIDO inaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wajasiriamali, ikiwemo ushauri wa kitaalamu, teknolojia za mashine, mikopo, mafunzo, masoko na uwekezaji, pamoja na kuwaunganisha wajasiriamali na fursa mbalimbali zinazolenga kuwawezesha kukuza biashara zao na hatimaye kuchangia katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. SIDO – PAMOJA TUJENGE VIWANDA
Matangazo
03 Dec, 2025
23 Nov, 2025
Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo