Utangulizi

Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 28 ya Mwaka 1973.
Shirika lilipewa majukumu ya kutoa huduma inayolenga kuwezesha uanzishwaji wa viwanda vidogo vinavyozingatia kuongeza thamani ya raslimali zilizoko nchini; Kuendeleza na kutumia teknolojia rahisi inayopatikana nchini; Kutoa kipaumbele kwa miradi ya uzalishaji inayotumia zaidi nguvu kazi;  Kuwezesha utengenezaji wa bidhaa za kutosheleza mahitaji ya wananchi hasa vijijini na ziada kuuza nje ya nchi;  Kushawishi, kuhamasisha na kusimamia uanzishwaji na uendelezwaji wa viwanda vidogo nchini.
 
Baadhi ya huduma zinazotolewa na Shirika ni; Huduma za kiufundi na maendeleo ya teknolojia, Uanzishaji wa miradi ya viwanda vidogo vijijini, Mafunzo, Ushauri na huduma za ugani, Masoko na Habari, na Huduma za fedha. 
 
Shirika linatoa huduma zake kwa kupitia mtandao wake wa ofisi za kutolea huduma zilizoko kila Makao Makuu ya Mikoa, zikiratibiwa na Ofisi Kuu iliyoko Dar es salaam. Shirika pia lina Mitaa ya Kuhudumia Viwanda Vidogo katika mikoa 18 na Vituo saba (7) vya Maendeleo ya Teknolojia.  
 
Shirika pia linajishughulisha na utekelezaji wa miradi maalumu kama Kuimarisha utoaji huduma vijijini kwa kutekeleza mkakati wa Wilaya Moja Bidhaa Moja (ODOP), Kuimarisha uwezo wa Usindikaji wa vyakula na Mradi wa Kuendeleza Ujasiriamali Vijijini (MUVI).