CHAMA CHA WAZALISHA SABUNI NA VIPODOZI CHAANZISHWA

Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ni miongoni mwa wazalishaji wa sabuni na vipodozi bila  ya kuwa na chama cha kuwaleta pamoja wazalishaji hao, hivyo katika kuleta mshikamano na kuchochea ukuaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kumeanzishwa chama cha wazalishaji hao kinachojulikana kama “Cosmetics and Soaps Manufacturer Tanzania (COSOMATA) chenye usajili Na. S.A. 23289 uliotolewa July 25, 2023.

Madhumuni makuu ya chama in pamoja na kushirikiana katika kumiliki viwanda vya uzalishaji wa sabuni na vipondozi: kuhamasisha wanachama waweze kuongeza uzalishaji wa bidhaa bora kwa kuwapatia mafunzo na mitaji; kusaidia wanachama kuzalisha na kuagiza malighafi za ndani na nje ya nchi; kuwa sauti ya wanachama ktika masuala mbalimbali yanayohusu uzalishaji na usambazaji wa sabuni na vipodozi; kusaidiana katika utafutaji wa malighafi za kutengenezea mafuta na sabuni kwa wanachama wake; kutoa elimu ya ujasiriamali ili kujenga ustawi wa wanachama wake.

Kutokana na umuhimu wa chama hiki, mnamo tarehe 31/01/2024, wanachama na wasio wanachama wa COSOMATA kwa kushirikiana na SIDO walikutaka  ili waweze kujadili mambo yahusianayo na chama ikiwemo taratibu za kujiunga na chama hiki na namna ya kuhamasisha wasio wanachama kujiunga ili wazalishaji wa bidhaa hizi waweze kufaidi fursa mbalimbali zitakazokuwemo ndani ya chama.

Sambamba na kikao hiki, wanachama waliweza kupata semina kutoka kwa Prof. Emmanuel Munishi wa CBE kuhusiana na mbinu za biashara na ujasiriamali; mikakati ya uendeshaji wa biashara na mbinu za masoko; maendeleo na mawasiliano ya kibiashara; na huduma kwa wateja. Pia waliweza kuelezewa  juu ya namna nzuri ya kufungasha ikiwemo branding, chaguzi sahihi za vifungashio pamoja na uwekaji sahihi wa lebo.