MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUNGANO WA TANZANIA AFUNGA MAONESHO YA NNE YA SIDO KITAIFA -NJOMBE, 2023

Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) katika moja ya huduma zake, ni kuhakisha bidhaa za wajasiriamali zinapata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi. Mnamo tarehe 21 Octoba hadi 31 Octoba, SIDO kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, ilifanya maonesho ya nne ya SIDO Kitaifa mkoani Njombe, yakiwa na lengo la kuonesha bidhaa mbalimbali zilizoongezwa thamani na zinazozalishwa na wajasiriamali wadogo na wa kati, zikiwemo bidhaa za uhandisi, nguo, sabuni, vipodozi, ngozi na bidhaa za dawa za asili. Maonesho haya yalifunguliwa rasmi na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaudi Kigahe mnamo tarehe 23/10/2-23.

Maonesho haya yaliahirishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dr. Isdor Mpango tarehe 28/10/2023. Katika hotuba yake, Mheshimiwa Makamu wa Rais, aliipongeza SIDO namna inavyowasaidia wajasiriamali wadogo na wa kati katika kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo nchini.  Aliziomba taasisi za fedha kuweka masharti nafuu ya mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati ambao wapo tayari kuanzisha  na kuendeleza viwanda vidogo.

Pamoja na kuipongeza SIDO, aliwaomba  kuangalia pia eneo la vifungashio na ufungashaji  kwa kuwa ni muhimu sana katika  kuongeza thamani malighafi mbalimbali zinazozalishwa hapa nchini na  hivyo inapaswa kupewa umuhimu wa kipekee. Mheshimiwa Makamu wa Rais aliwataka SIDO kutafakari kuanzisha tuzo za wabunifu wa mashine mbalimbali za kuongeza thamani  na pia kuwazawadia tuzo wazalishaji bora wa viwanda vidogo na vya kati ambapo inaweza kuwa ni vyeti au kuwapatia kiasi fulani cha fedha kama motisha wa kazi nzuri wanazofanya katika kuendeleza viwanda vidogo nchini.

Katika kuhakikisha SIDO inafungu la kutosha katika kutekeleza majukumu yake, Ili  Mheshimiwa Makamu wa Rais aliiomba Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha kipindi cha bajeti SIDO inatengewa fungu kubwa litakalowawezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Pia aliongeza kuwa, pamoja na majukumu kuwa mengi, SIDO inaweza kuomba taasisi nyingin kuwasaidia kutekeleza baadhi ya majukumu.

Makamu wa Rais alitumia fursa hiyo kuwashukuru Wizara ya Viwanda na Biahara kwa kumwalika kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha Maonesho ya nne ya SIDO Kitaifa. Pia kwa namma ya pekee, alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka pamoja na timu yake nzima  kwa kukubali kufanya maonesho hayo mkoani Njombe. Pia   aliipongeza menejimenti na wafanyakazi wote wa  SIDO kwa kuendeleza utamaduni wa kuvumisha bidhaa za wajasiriamali zikiwemo teknolojia mbalimbali za mashine. Alizipongeza pia taasisi zilizoshiriki katika maonesho haya, wajasiriamali kutoka mikoa mbalimbali pamja na wananchi wote kwa ujumla.