MAONESHO YA NNE YA SIDO KITAIFA NJOMBE, YAIBUA WABUNIFU WA TEKNOLOJIA MBALIMBALI.

Maonesho ya Nne ya SIDO ya Kitaifa yaliyoandaliwa na  Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO)  kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, yalihudhuriwa na wajasiriamali wadogo na wa kati kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani. Maonesho haya yalikuwa yamesheheni bidhaa mbalimbali za wajasiriamali zikiwemo teknolojia za mashine zilizokuwa zimetengenezwa kwa ubunifu mkubwa.
Mkoa wa Njombe ni miongoni mwa  mikoa inayosifika kwa kuwa na wajasiriamali wenye ubunifu mkubwa hasa kwenye maswala ya teknolojia. Ni mkoa  uliojipatia umaarufu mkubwa kutokana na wananchi wake kuwa kwenye tano bora ya mikoa iliyo na kipato cha kati. Pia ni mkoa ulio na malighafi nyingi zinazohitaji kuongezewa thamani. 

Kijana Estomin Eston Chaula ni  mmoja wa wabunifu wa Njombe  aliyeshiriki maonesho haya  na ambaye aliweza kuonyesha ubunifu wake kwenye utengenezaji wa magari, sensor na generator. Gari alilotengeneza mbunifu huyu lilikuwa linalotumia engine ya mashine ya kusaga nafaka. Moja ya sifa kubwa ya gari hili, ni nguvu kubwa iliyonayo ya kubeba mzigo mkubwa kutokana na kufungwa gear box mbili.
Pia kulikuwepo na trekta ndogo lililokuwa na uwezo wa  kulima mashamba. Trekta hili lina uwezo wa  kutumika  kumwagilia mashamba kwa kufungwa pampu ya maji;  kutumika kama chombo cha kufua umeme;  kufungwa jembe la kulimia shambani;  na kutumika kama reki.   Trekta hili linatumia mafuta kidogo na linaweza kutumika pia kama  mashine ya kusaga nafaka mbalimbali.

Mbunifu huyu alikua pia  na sensor mbalimbali ikiwemo ya kufukuzia  wadudu na wanyama waharibifu wa mazao kama vile ndege na panya pori n.k. Sensor hii ni lulu kwa wakulima kwa kuwa inatumia  nishati  ya jua (solar). Moja ya sifa  kubwa ya sensor hii ni kubadili kwake  mlio kunapojitokeza kwa  mazingira hatarishi huku ikiendelea kujichaji. Sensor nyingine ni ya ulinzi  wa nyumba ambapo hutuma ujumbe kwa mhusika  kupitia simu yake ya mkononi  endapo kutakuwa na shida yeyote.

Mbunifu huyu pia alibuni generator  inayotumia gesi ya kupikia tofauti na za sasa zilivyo ambazo zinatumia  petrol au diesel.  Inatunza mazingira  kutokana na kwamba haitoi moshi, ina stabilize na matengenezo yake ni machache.