MAONESHO YA NNE YA SIDO KITAIFA YAWA CHACHU ZA UTAMBUZI WA FURSA ZILIZOPO MKOANI NJOMBE.

MAONESHO YA NNE YA SIDO KITAIFA YAWA CHACHU ZA UTAMBUZI WA FURSA ZILIZOPO MKOANI NJOMBE.

Katika kuwezesha bidhaa za wajasiriamali kutambulika ndani na nje ya nchi, SIDO iliandaa maonesho ya nne ya Kitaifa yaliyofanyika mkoani Njombe kuanzia tarehe 21 hadi 31 Oktoba, 2023. Maonesho haya yalihudhuriwa na wajasiriamali takribani 500 wakiwa na bidhaa mbalimbali zikiwemo bidhaa za uhandisi, vyakula, nguo, ngozi, madawa ya asili na bidhaa za sabuni na vipodozi.

Maonesho haya yalifunguliwa rasmi na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud S. Kigahe. Katika maelezo yake, Mhe. Kigahe alionyesha namna serikali inavyotambua mchango wa viwanda vidogo katika kuinua uchumi na kutoa ajira endelevu. Alieleza kuwa, zaidi ya ajira milioni 8 zinatokana na viwanda vidogo. Na pia aliongeza kuwa, fursa nyingi za biashara zinaweza kuibuliwa kutokana na maonesho haya zikiwemo teknolijia mbalimbali za kusindika, kuchakata na kuchechua madini mbalimbali.

Fursa zilizopo mkoani Njombe zilielezewa vyema na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Bi. Kisa Bwakisa zikiwemo uwekezaji kwenye madini kama makaa ya mawe huko Ludewa, Mchuchuma; uwekezaji kwenye kilimo cha maparachichi, apples; uwekezaji kwenye mbao na nguzo; uwekezaji kwenye utalii – Kitulo na uwekezaji Baridi. Mkuu wa Wilaya aliainisha takwimu za viwanda mkoani Njombe na kuonyesha kuwa, vipo viwanda 977 vidogo; viwanda vikubwa ambavyo vinatumia malighafi ya viwanda vidogo vipo 13; viwanda vya kati vipo 67 na viwanda vidogo sana vipo 667. Aliongeza pia, mkoa wa Njombe unasifika kwa kuwa na Amani na utulivu, miundo mbinu imara na kuwa mkoa wa tano kitaifa katika kundi la mikoa wa watu wenye kipato

Mkurugenzi wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji, alisisitiza watanzania kupenda kutumia bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa kwa kutumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini ili kuinua uchumi wa Tanzania. Aliongeza kuwa, SIDO inazo karakana (TDCs) zinazotengeneza mashine mbalimbali nzuri na za kisasa kwa ajili ya kusindika na kuchakata malighafi mbalimbali kwa ajili ya kuongeza thamani. Hivyo hatuna budi kutumia teknolojia hizi kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbalimbali zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.