Mkakati wa Wilaya Moja Bidhaa Moja (ODOP)

Ni mkakati unaolenga kujenga uwezo wa uongezaji thamani ya raslimali zilizopo wilayani na hasa vijijini na kuchangia juhudi za kupunguza umaskini. 
 
Mkakati huu ulitayarishwa kutokana na dhana ya Kijiji Kimoja Bidhaa Moja (OVOP) kutoka Japan katika wilaya ya Oita iliyoanzishwa mwaka 1970. Nia hasa ya dhana hii ni kuwajengea uwezo wananchi kwa kupitia vikundi kutumia raslimali walizonazo kuanzisha viwanda vidogo vya kuongeza thamani, kuongeza nafasi za kazi, kuongeza kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi ulio endelevu.
 
Kwa Tanzania, mkakati unalenga kuimarisha utoaji wa huduma katika karibu maeneo yote unaozingatia kumjengea uwezo mjasiriamali mdogo ili kuongeza ufanisi na tija katika shughuli zake za uzalishaji na biashara, kuongeza kipato, utambulisho na sifa kwa wananchi wa maeneo husika. 
 
Uongezaji thamani katika raslimali unaimarishwa kwa kuwezesha uzalishaji, udhibiti wa ubora wa bidhaa na kuhakikisha upatikanaji wa vifungashio vifaavyo na kuwezesha bidhaa hizo kufanya vizuri kwenye masoko.Utekelezaji wa mkakati huu hufanywa kwa ushirikiano wa wakulima, wasindikaji na Serikali za Mitaa kwa wahusika wakuu, na kupata michango ya utaalamu na uwezeshaji kutoka SIDO na wadau wengine.