PATA TAARIFA MBALIMBALI KUPITIA MITANDAO YA SIDO

PATA TAARIFA MBALIMBALI KUPITIA MITANDAO YA SIDO

Katika kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia  ya utandawazi, Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) limeendelea kutumia njia mbalimbali za mawasiliano ili kutoa taarifa zinazohusu Shirika na huduma zake. Njia zinazotumika  katika utoaji taarifa mbalimbali ni pamoja na tovuti ya Shirika, mitandao ya kijamii kama facebook (sidotanzania), twitter(sidotanzania) na instagram(sido_tanzania).  Mambo yanayotumwa katika mitandao hii ni pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na SIDO zikiwemo teknolojia mbalimbali za mashine, ratiba za mafunzo, bidhaa za wajasiriamali na taarifa juu ya mifuko ya uwezeshaji. Kwa upande wa mafunzo, SIDO imekuwa inatoa mafunzo mbalimbali yanayolenga kuongeza thamani baadhi ya malighafi zinazozalishwa hapa nchini pamoja na namna ya kuanzisha, kuendeleza na kumiliki kiwanda kidogo. Mafunzo hayo ni pamoja na usindikaji wa vyakula, utengenezaji wa sabuni, vipodozi, namna nzuri ya kufungasha na mambo ya kuzingatia katika ufungashaji wa bidhaa na mengine mengi.

Katika huduma za kifedha, SIDO imekuwa ikitoa mikopo na ushauri wa kifedha kupitia mifuko yake ya NEDF, RRF, SANNV na CGS.  Wanufaika wa mifuko hii ni wajasiriamali wadogo na wa kati.
Mfuko wa kuendeleza  wananchi kiuchumi (NEDF) umekuwa unatoa mkopo wa juu wa kiasi cha Sh.5,000,000 ukiwa na riba ya asilimia 9%. Sifa za mwombaji ni lazima  awe anajishughulisha na shughuli za uongezaji thamani malighafi mbalimbali na  awe na wadhamini ( 2 ) wenye dhamana ya nyumba , gari au kiwanja. 

Kwa mfuko wa SANNV,  unatoa mkopo kwa wajasiliamali wenye sifa zifuatazo:
• Mkopaji awe amewahi kutumia huduma yoyote ya SIDO,
• Uwe na  kiwanda kilichodumu kwa Zaidi ya mwaka mmoja na kinachoendelea na uzalishaji.
• Mjasiriamali anaweza kukopeshwa  hadi milioni 200, na riba  yake ni  13%  mwaka mmoja  ambapo anaweza kuulipa ndani ya  miaka saba.
Mfuko wa CGS unamtaka mkopaji  awe na mradi wa kuongeza thamani malighafi mbalimbali;  awe na uwezo wa kukopa  kuanzia milioni 10 hadi 50 na alipe ndani ya miaka 3.  Na pia awe ameshawahi kupata huduma yeyote ya SIDO

Mfuko wa mzunguko wa mkoa (RRF), mjasiliamali anaweza kukopa hadi milioni 6.5 milioni 6.5 na Riba yake ni 22% ambayo  atatakiwa kulipa ndani ya miaka 3. Mjasiliamali pia anaweza kuunganishwa na Taasisi mbalimbali za kifedha ili kupata mkopo kwa riba nafuu  na uharaka wa huduma.  
Katika kuendeleza Teknolojia na viwanda,  SIDO Kupitia tovuti na mitandao yake ya kijamii imekuwa ikionyesha  mashine mbalimbali za kuongeza thamani kutoka Vituo vyake vya Kuendeleza Teknolojia (TDCs) pamoja na za wajasiriamali. SIDO inavyo vituo saba vya kuendeleza teknolojia katika mikoa ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Kigoma, Iringa, Shinyanga na Lindi. Vituo hivi hunatengeneza mashine za aina tofauti tofauti ili kurahisisha shughuli za  usindikaji na uchakataji wa bidhaa mbalimbali.    Mashine hizo ni pamoja na  mashine za kuchakata ngozi, kusindika  karanga, kusaga vitu mbalimbali, mashine za juisi, miwa n.k   

Kwa maelezo zaidi kuhusu upatikanaji wa mashine na bidhaa mbalimbali,  mafunzo, upatikanaji wa mikopo usisite kuwasiliana na SIDO iliyo karibu nawe