SIDO ARUSHA YAFANYA MAFUNZO JUU YA VIFUNGASHIO NA UFUNGASHAJI KWA WAJASIRIAMALI

SIDO imeendelea kuwaelimisha  wajasiriamali wadogo na wa kati  katika nyanja mbalimbali ili  kuwapatia ujuzi wa kuongeza thamani malighafi zinazozalishwa hapa nchini.  Sambamba na ujuzi huo, pia wajasiriamali wanaendelea kupatiwa mafunzo juu ya namna nzuri ya kufungasha ikiwemo uwekaji taarifa muhimu kwenye lebo na chaguzi sahihi za vifungashio.  

Hivi karibuni, Meneja wa SIDO Arusha aliandaa  mafunzo ya  Branding, Packaging  na Labelling kwa wajasiriamali takribani 40 wanaozalisha bidhaa mbalimbal yakiwa na lengo la kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kufungasha bidhaa zao ili ziwe na  mwonekano mzuri na wakuvutia katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mafunzo haya yameanza kutolewa kwa wajasiriamali baada ya kuona kuwa, wapo baadhi ya wajasiriamali ambao wamekuwa wanafungasha bidhaa zao bila kuzingatia  kanuni muhimu za ufungashaji ikiwemo chaguzi sahihi za vifungashio, uwekekaji taarifa muhimu kwenye lebo,    uandishi  wa  vipimo usio sahihi,  uwekaji tofauti wa alama za utambuzi wa bidhaa na mambo mengine mengi. Ili kuyaongezea uzito mafunzo haya, SIDO iliweza taasisi  husika zinazoshughulika moja kwa moja na maeneo tajwa ambao ni za  BRELA,  GSI Tz, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Vipimo (WMA). Wawakilishi toka katika taasisi hizi waliweza kuwaelimisha wajasiriamali  waliohudhuria mafunzo haya kuhusiana na maswala mbalimbali juu ya vifungashio na ufungashaji.

Mafunzo haya  yalikuwa ya siku mbili na yalikuwa na mwitikio mkubwa ambapo wajasiriamali waliweza kutambua makosa mbalimbali wayafanyao  katika ufungashaji na hivyo kuahidi kutumia elimu waliyopata katika kuboresha bidhaa zao. Mafunzo haya yalifungwa rasmi na Afisa Biashara wa Mkoa wa Arusha, Frank  Mmbando, ambapo washiriki waliweza kupatiwa vyeti vya ushiriki na kusisitizwa kutumia elimu waliyoipata ili bidhaa zao ziweze kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.

SIDO itaendelea na mkakati wa kutoa mafunzo haya kupitia ofisi zake katika mikoa yote Tanzania bara ili kuhakikisha wajasiriamali wanaendelea kuboresha mwonekano wa bidhaa zao na hivyo kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.