Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo ( SIDO ) limeendelea kujizolea sifa na umaarufu mkubwa kutokana na huduma zake kwa wajasiriamali na hususani vituo vyake vya kuendeleza teknolojia (TDC). Vituo hivi vimekuwa chachu ya uanzishaji viwanda vidogo kwa kuwa mashine mbalimbali za usindikaji na uchakataji malighafi mbalimbali zimekuwa zinazalishwa kupitia vituo hivi.
Tanzania imejaliwa kuwa na malighafi mbalimbali zinazotokana na kilimo, ufugaji na uvuvi. Malighafi hizi zinahitaji kuongezea thamani ili bidhaa mbalimbali ziweze kuzalishwa. Uongezaji thamani malighafi hizi unahitaji teknolojia mbalimbali za uzalishaji. Hii ilipelekea SIDO kuanzisha vituo vya kuendeleza teknolojia vijulikanavyo kama TDC.
SIDO TDC zipo kwenye mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Kigoma, Iringa, Lindi na Shinyanga. Kupitia vituo hivi, teknolojia mbalimbali zimekuwa zinazalishwa kulingana na malighafi zinazopatikana katika mikoa husika na hivyo kuongezwa thamani. Hii imepelekea kuzalishwa kwa mashine kama mashine za kuchakata ngozi, kusaga karanga, kusaga mahindi, kusindika kahawa, kuchakata mihogo, kufyatua matofali, kukamua juisi, n.k
Wajasiriamali wameweza kufaidika na vituo hivi na hivyo:
wajasiriamali wabunifu wameweza kuboresha mashine zao kwa kushirikiana na vituo hivi ambavyo vimekuwa pia vinatengeneza vipuri mbalimbali kwa ajili ya kutengenezea mashine.
wajasiliamali wanaozalisha mashine mbalimbali wamekuwa wanapewa ushauri wa kiufundi.
Kutokana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na Teknolojia, SIDO imekuwa inaagiza mashine kutoka nje ya nchi ili wajasiriamali wenye uhitaji waweze kununua kwa ajili ya kuongeza thamani malighafi zao.
Vituo hivi vimekuwa vinawasaidia wahunzi katika wanaboresha wa vifaa vyao na hivyo kuwa chanzo cha upatikanaji vifaa vingi vinavyotokana na chuma kama vile majembe, mashoka, mapanga, n.k
Vipuri mbalimbali vimekuwa vinachongwa kutoka kwenye vituo hivi vikiwepo pia vipuri vya magari, mashine nyingine nyingi n.k
Vituo hivi vimekuwa vinatengeneza mashine kulingana na mazao yaliyoainishwa kupitia program ya Bidhaa Moja Wilaya Moja (ODOP) na hivyo kurahisisha utengenezaji wa mashine na uanzishwaji wa viwanda kwa kasi kupitia wilaya zote ziliyopo katika kila mkoa.