SIDO YAITISHA JUKWAA LA WADAU WAZALISHAJI WA VIFUNGASHIO NA WAJASIRIAMALI

SIDO YAITISHA JUKWAA LA WADAU WAZALISHAJI WA VIFUNGASHIO NA WAJASIRIAMALI

Katika kuhakikisha changamoto ya vifungashio inayolalamikiwa na wajasiriamali walio wengi imepata suluhu, SIDO iliandaa jukwaa la  wadau wazalishaji wa vifungashio mbalimbali pamoja na wajasiriamali  ili kuweza kubaini mahitaji, changamoto na fursa mbalimbali zilizopo kwenye sekta hii ya vifungashio na ufungashaji.  Jukwaa hili lilihudhuriwa na wajasiriamali zaidi ya 60 pamoja na  makampuni  8 yanayozalisha vifungashio mbalimbali kutoka mikoa ya Dar Es Salaam na Pwani

Mafunzo  mbalimbali yanayotolewa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO),yamewafanya  watanzania wengi kuhamasika na hivyo  kuanzisha viwanda vidogo  vya kuongeza thamani malighafi zinazopatikana hapa nchini. HIi imepelekea uzalishwaji wa bidhaa mbalimbali zilizosindikwa au kuchakatwa zikiwemo bidhaa za vyakula, sabuni, vipodozi, ngozi, nguo n.k.  Licha ya bidhaa hizi kuzalishwa kwa kuzingatia ubora na usalama kwa mtumiaji, tafiti mbalimbali  zilizofanywa na wataalamu wetu zimebaini kuwa, bidhaa hizi za  hasa za vyakula, vipodozi na sabuni hazipo kwa wingi kwenye  masoko ya nje ukilinganisha na nchi nyingine. Sababu mojawapo iliyotajwa ni ufungashaji hafifu na uchaguzi usio sahihi wa vifungashio unaopelekea bidhaa kutovutia kwenye masoko ya ndani na  nje ya nchi.

SIDO kama mtoa huduma mbalimbali kwa wajasiriamali, iliamua kuja na mkakati wa kuitisha jukwaa la kuwakutanisha baadhi ya wazalishaji wa vifungashio  na wajasiriamali ili kuweza kubaini changamoto zilizopo kwa pande zote mbili lengo likiwa ni kutengeneza mikakati madhubuti ya kupunguza au kutatua changamoto hiyo hatimaye kuzifanya bidhaa za wajasiriamali kuweza kupata masoko ndani na nje ya nchi.
Katika jukwaa hilo, wajasiriamali walitoa  baadhi ya  changamoto wanazokumbana nazo ambazo ni;-
• Ukosefu wa aina tofauti tofauti ya vifungashio unaopelekea bidhaa kufanana sana na hata kupelekea aina  fulani ya kifungashio  kutumiwa kwa bidhaa zaidi mbili
• Ubora hafifu kwa baadhi ya vifungashio vinavyozalishwa hapa nchini mfano kukunjika kwa haraka, kufubaa na kadhalika unaopelekwa baadhi ya wajasiriamali kuagiza kutoka nje na hivyo kufanya bidhaa husika kuwa ya gharama kubwa
• Uchache  wa viwanda vya uzalishaji  vifungashio hasa vya kioo ambapo kwa sasa kiwanda kilichopo  kinazalisha vifungashio kwa ajili ya viwanda vinavyozalisha vinywaji mbalimbali kama  soda, mvinyo na bia
• Wasambazaji wa vifungashio kuwa mbali na wahitaji hivyo kusababisha ongezeko la gharama katika uzalishaji
• Mtaji mdogo wa kuendesha biashara hali inaosababisha kushindwa kununua vifungashio kwa bei ya jumla
Wazalishaji wa vifungashio walieleza  changamoto zao ambazo ni gharama kubwa ya uwekezaji katika  sekta hii; uhitaji wa vifungashio kwa wajasiriamali kuwa  chini kwa kuwa wengi wanahitaji vifungashio vya bei nafuu; gharama za uendeshaji kuwa juu mfano umeme, maji, na nyinginezo. Pia kukosekana kwa umeme wa kuaminika ambapo huwasababishia hasara kubwa pindi unapokatika ghafla wakati uzalishaji undaendelea. Gharama nyingine kubwa ni utengenezaji maumbo mbalimbali ya vifungashio (molds) na uwezo wa mjasiriamali kugharamia pamoja na ununuzi wa malighafi za uzalishaji vifungashio (preforms).  Taratibu za kusajili biashara zimekuwa za mlolongo mrefu ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vibali mbalimbali katika  mfano OSHA, NEMC, GCLA, FIRE, BRELA n.k

Pamoja na changamoto zilizobainishwa na wajasiriamali, SIDO inaendelea na  mikakati yake ya kuwahudumia wajasiriamali na hasa kwenye sekta hii ya vifungashio na ufungashaji ikiwemo;-
• Kuwakaribisha wazalishaji wa vifungashio kuwekeza kwenye maeneo ya SIDO mitaa ya viwanda;
• Kuwasogezea wajasiriamali  huduma ya vifungashio kwa kununua kwa jumla kutoka kwa wazalishaji wa vifungashio na kuwasambazia kupitia ofisi za SIDO Mikoa;
• Kuunganisha wajasiriamali na wazalishaji wa vifungashio hasa wale ambao mahitaji yao ni makubwa;
• Kuweka mawasiliano ya wadau wazalishaji wa vifungashio  kwenye tovuti ya Shirika, majarida mbalimbali ya Shirika, mitandao ya SIDO ya jamii na kwingineko;
• Kubuni na kutengeneza vifungashio kulingana na mahitaji ya wasindikaji.
• Kutoa ujuzi na ushauri katika maeneo ya Branding, Packaging and Labelling
• Kutumia mtandao wa SIDO ngazi ya wilaya, kongano za viwanda,  balozi wa huduma za SIDO (role model) katika usambazaji wa vifungashio.

SIDO tunaamini kuwa kupitia jukwaa hili ambalo ni mwendelezo wa majukwaa yajayo, wajasiriamali na wazalishaji wa vifungashio mbalimbali watawasiliana na kuwa na maono ya pamoja ya kupunguza changamoto ya vifungashio. Hii itasaidia pia na kupanua wigo wa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini  kupata masoko ya uhakika ndani  na nje ya nchi na hivyo kupelekea kukuza uchumi na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda.