SIDO YAVUMISHA BIDHAA ZA WAJASIRIAMALI KUPITIA MAONESHO YA KIMATAIFA YA 47 YA BIASHARA YA DAR ES SALAAM, 2023

Kupitia Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar Es Saam  yaliyofanyika  viwanja vya Nyerere, barabara ya Kilwa  kuanzia tarehe 28 Juni na kumalizika tarehe 13 Julai, 2023, SIDO ilihakikisha kuwa wajasiriamali walioshiriki maonesho hayo wanakukutanishwa na wadau mbalimbali na pia kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali kipindi chote cha maonesho. Mafunzo hayo yalikuwa mahususi kwa waoneshaji yakihusisha namna nzuri ya kupanga bidhaa, mawasiliano na wateja, maswala ya chaguzi sahihi za vifungashio kulingana na bidhaa wanazozalisha, maswala yote ya uwekaji chapa na taarifa muhimu zinazotakiwa kwenye lebo.

Takribani wajasiriamali 160 waliweza kushiriki kwenye maonesho hayo   kwenye banda la SIDO  vikiwemo vikundi  vilivyofadhiliwa na taasisi  mbalimbali kama vile JICA, USAID na MUAVI kupitia halmashauri za mikoa. Wajasiriamali hawa  walitoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania bara na Visiwani wakiwa na  bidhaa za ngozi, nguo, uhandisi, vyakula vilivyosindikwa, sabuni na vipodozi, na dawa mbalimbali za asili.
Wengi wao walinufaika sana na mafunzo mubashara yaliyokuwa yanatolewa   kwenye banda yakiwa yanahusisha wadau kutoka taasisi mbali mbali  zikiwemo WMA, TBS, BRELA na GSI Tz. Pia hii ilikuwa fursa nzuri kwao kuweza  kujifunza kwa wengine na kuona namna ambavyo wajasiriamali  wenye bidhaa kama zao walivyoweza kupiga hatua na kupata masoko ndani na nje ya nchi.

SIDO, kupitia Vituo vyake vya Kuendeleza Teknolojia (TDCs) iliweza kuleta mashine mbalimbali za kuongeza thamani malighafi zinazozalishwa hapa nchini zikiwemo mashine za kusindika karanga, nyama, kusaga, kuchakata ngozi, kuchachua madini n.k. Wajasiriamali  waliokuwa tayari kuanzisha viwanda vidogo na vya kati   waliweza kujipatia mashine hizi ambazo zimetengezwa kwa ufanisi mkubwa ili kumwezesha mjasiriamali kuzalisha bidhaa bora na zenye viwango.    Wageni kutoka taasisi mbalimbali, balozi na wastaafu mbalimbali walikuwa miongoni mwa watembeleaji wa maonesho haya kwenye banda la SIDO. 

Ili kuzidi kuvumisha bidhaa hizi za wajasiriamali, SIDO imeandaa maonesho makubwa ya kitaifa yanayojulikana kama Maonesho ya 4 ya SIDO Kitaifa ambayo yanategemewa kufanyika katika mkoa wa Njombe kuanzia tarehe 21/10/2023 hadi 31/10/2023. Wajasiriamali kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani wanakaribishwa kwa kuwa, SIDO pia  itaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Eng. Prof. Sylvester Mpanduji  aliwapongeza wajasiriamali wote kwa kushiriki kikamilifu kwenye maonesho haya na vilevile aliwapongeza viongozi, wananchi na wadau wote walioweza kutembelea  maonesho kwenye banda la SIDO.