SIDO imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wajasiriamali wanapatiwa mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kuongezaji thamani malighafi zinazozalishwa au kupatikana hapa nchini. Uongezaji thamani huu umepelekea kuanzishwa kwa viwanda vidogo na vya kati ambavyo vimekuwa vinatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda na uchumi kwa ujumla. Sambamba na mafunzo haya ya uongezaji thamani, SIDO imeendelea pia kutoa mafunzo juu masoko ikiwemo uwekaji chapa, ufungashaji na uwekaji lebo (branding, packaging and labeling) yakiwa na lengo la kuwawezesha wajasiriamali kufungasha vyema bidhaa zao ili kuweza kuvutia masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mafunzo ya siku mbili ( 20 na 21 Februari, 2024) juu ya uandaaji chapa (branding), ufungashaji na uwekaji lebo yaliandaliwa na kutolewa kwa wajasiriamali wanaozalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo bidhaa za vyakula vya kusindikwa, sabuni na vipodozi n.k. Mafunzo haya yalihusisha pia taasisi za TBS, BRELA, WMA, GSI Tz na Scan Code kwa kuwa kwa namna moja au nyingine wanahusika kwenye utoaji elimu juu vifungashio, ufungashaji na uwekaji taarifa muhimu kwenye leo.
Washiriki walifurahia sana mafunzo haya kwa kuwa yaliwawezesha kutambua vitu mbalimbali kuhusiana na ufungashaji vikiwemo, namna ya kufanya uchaguzi sahihi za vifungashio kulingana na bidhaa wanazozalisha, taarifa muhimu zinazotakiwa kwenye lebo, namna ya kuchagua na kusajili majina ya biashara, uandishi sahihi wa vipimo, uundaji wa chapa na vitu vya kuzingatia n.k