WAZIRI MKUU AFANYA ZIARA SIDO KIGOMA.

WAZIRI MKUU AFANYA ZIARA SIDO KIGOMA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amefanya ziara Mkoani Kigoma ikiwa na lengo la kufanya tathimini ya mafanikio ya mkakati wa kuendeleza zao la mchikichi mkoani humo. Zao la mchikichi ni moja ya zao la kimkakati ambalo limepewa msukumo mkubwa na Serikali ya awamu ya sita ili kuondoa uhaba wa mafuta ya kula nchini.

Ziara hiyo mkoani Kigoma ilitanguliwa na mkutano wa wadau mbalimbali wanaojihusisha na zao la mchikichi wakiwemo wazalishaji wa mbegu, wakulima na wachakataji wa zao la mchikichi. Katika mkutano huo wa tathimini; ilionesha kuwa,  mbegu ambazo zimezalishwa na TARI pamoja na ASA zimethibitisha kuwa na ubora na kwamba zinatoa  matunda kati ya miaka miwili hadi mitatu.
Waziri Mkuu, alipata fursa ya kutembelea mtaa wa Viwanda SIDO Kigoma  ili kujionea viwanda mbalimbali vinavyojihusisha na uongezaji thamani wa zao la Mchikichi.  Katika ziara hiyo Mhe. Waziri Mkuu alikaribishwa na Mkurugenzi Mkuu wa SIDO Mhandisi. Profesa Sylvester Mpanduji kwenye kiwanda cha kukausha mbegu za chikichi (mise). Meneja wa Mkoa- SIDO Kigoma, Bw. Gervas Ntahamba, alitoa maelezo kuhusu  miradi mbalimbali inayofanywa na SIDO kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika uongezaji thamani wa zao la mchikichi.

Mheshimiwa Waziri Mkuu aliweza kujionea mtambo wa kukausha mise unavyofanya kazi na kwamba unakwenda kuondoa changamoto ya ukaushaji wa mbegu hizo kwa muda mrefu. Kwa sasa mbegu hizo huanikwa juani na huchukua muda wa siku 3 hadi 5 ili kuweza kukauka kwa jua, kupitia mtambo huu inachukua saa moja tu kuweza kukausha mbegu hizo. Mtambo una uwezo wa kukausha tani 3 hadi 15 kwa saa moja. Mradi huu umefadhiliwa na UNCDF chini ya Programu ya UN Kigoma Joint Program na sasa  unamilikiwa na SIDO kwa asilimia 60 na Ushirika wa akina mama Wajasiriamali SIDO  kwa asilimia 30 na asilimia 10 zimewekwa ili zije kuongeza mtaji baadaye kwa kuziuza. Pia aliweza kujionea mashine ya kukamua mafuta na kuchuja mafuta ya Mise ambayo ni sehemu ya mradi wa kukausha mbegu za chikichi. 
Katika matembezi yake mtaa wa viwanda SIDO Kigoma, Mhe. Waziri Mkuu aliweza kukutana na wadau wengine  wanaojihusisha  na mnyororo wa zao la mchikichi ambapo  alitembelea kiwanda cha kati cha kukamua mafuta ya mawese na kuyasafisha mafuta hayo.  Mkurugenzi wa Kampuni ya Trolle Messle Bw. Abdul Mwilima na Mkurugenzi wa Uendeshaji Bw. Daniel Amulike waliweza  kutoa maelezo  ya namna mitambo hiyo itakavyofanya kazi mara baada ya shughuli ya kusimika mitambo hiyo kukamilika.

Mwisho, Mhe. Waziri Mkuu alipongeza uongozi wa Mkoa, SIDO na wadau wengine kwa hatua walizochukua hadi sasa. Aidha aliagiza  SIDO kuendelee kubuni na kutengeneza teknolojia za kisasa  ambazo  zitasaidia ufanisi katika uchakataji wa zao hilo.

Katika hatua nyingine alipiga marufuku utumiaji wa vipimo visivyo sahihi maarufu BIDOO vinavyotumiwa na wanunuzi wa mafuta ya mawese. Alielekeza vipimo vilivyotengenezwa na SIDO Kigoma vitumike mara moja.