Hivi karibuni, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Ashatu K. Kijaji akiwa ameongozana na Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Hashil T. Abdallah, walizindua Bodi mpya ya Wakurugenzi - SIDO. Uzinduzi huu unakuja baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumteua Mhand. Mussa A. Nyamsigwa, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya SIDO.
Katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya SIDO, Mhandisi. Mussa A. Nyamsigwa, alimpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuamini na kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya SIDO. Aliongeza kuwa, anajua umuhimu wa SIDO na mwamko wananchi walionao katika kuendeleza viwanda vidogo nchini. Ili kusaidia katika kuinua uchumi wa nchi kupitia SIDO, aliahidi kuitumia nafasi yake kama Mwenyekiti katika kushauri na kuwasaidia wananchi wengi kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo nchini.
Mwenyekiti wa Bodi aliiomba Serikali kupitia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, iendelee kuiimarisha SIDO kwa rasilimali watu, vitendea kazi n. k ili Shirika lizidi kujizatiti na kufikia malengo yake. Aliongeza kuwa, katika utendaji wake wa kazi na SIDO, atahakikisha mazingira ya utoaji wa huduma yameimarishwa na pia mahitaji halisi na thamani halisi ya kifedha zitakazotumika yanazingatiwa. Mwenyekiti wa Bodi wa SIDO kwa kushirikiana na wajumbe wengine wa Bodi walionyesha utayari wa kushirikiana na Menejimenti ya SIDO bega kwa bega ili kufanya utendaji wa Shirika usikwame.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji, alipata fursa ya kuelezea kwa mapana huduma mbalimbali zinazotolewa na SIDO katika kuwawezesha wajasiriamali nchini kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo na vya kati. Alizitaja baadhi ya hizo zikiwemo maendeleo ya teknolojia na ufundi; mafunzo kwa wajasiriamali na huduma za ugani; masoko na uwekezaji pamoja na utoaji wa mikopo. Huduma hizi hutolewa katika Mikoa yote ya Tanzania Bara kupitia Ofisi zake za SIDO zilizopo katika kila mikoa.
Pamoja na mambo mengine, Mkurugenzi Mkuu wa SIDO alionyesha mipango mikakati ya Shirika ikiwemo:-
• Kuhawilisha Teknolojia kwa wingi kupitia vituo vyake vya uendelezaji teknolojia ( TDCs) na kuendelea kuviimarisha huku ikianzisha vituo vingine vipya.
• Kuongeza wigo wa huduma za SIDO Kwa wajasiriamali kwa kutoa mafunzo, ushauri na huduma za Ugani kupitia TEHAMA na uimalishaji wa vituo wa Mafunzo na Uzalishaji ( NTPC )
• Kuendeleza mitaa ya Viwanda ya SIDO kwa kuweka miundombinu wezeshi na kukamilisha kutengeneza mfumo unganishi wa TEHAMA kwa Shirika ili kurahisisha mawasiliano ya kidigitali kwa ofisi zote za shirika.
• Kuimarisha mfuko wa kuendeleza wajasiriamali kifedha kupitia mfuko wake wa NEDF.
• Kutangaza huduma za Shirika na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wajasirimali.
• Kuongeza idadi ya watumishi, kutoa motisha na kuwapatia Mafunzo ili kuendana na mabadiliko ya Teknolojia na kuongeza ufanisi kwa kuwapatia vitendea kazi ili kuhakikisha huduma zinawafikia walengwa kwa wakati.
• Kuimarisha ushirikiano na wadau/ mashirika ya kitaifa na kimataifa kwa lengo la kuzidi kuimarisha huduma zetu na kulijengea uwezo Shirika.