Hivi karibuni, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Suleimani Jafo, alifanya ziara katika Ofisi za Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) - Upanga kwa lengo la kujitambulisha na kusalimiana na wafanyakazi. Katika ziara yake, Mhe. Dkt. Jafo aliambatana na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara (Mhe. Balozi Dkt John Simbachawene), Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara (Sempeho Manongi) na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda ( Juma Mwambapa).
Katika hotuba yake aliipongeza sana SIDO kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya katika kuwahudumia wajasiriamali wadogo na wa kati. Alionyesha namna wajasiriamali wenye bidhaa mbalimbali na zenye viwango wanavyojitahidi kushiriki maonesho mbalimbali yakiwemo yale yanayoandaliwa na SIDO na wadau mbalimbali wa maendeleo. Alieleza kuwa, wazalishaji bidhaa mbalimbali wana matarajio makubwa sana na SIDO wakiwemo wakulima na wavuvi na hasa kwenye maswala ya mafunzo mbalimbali ya uongezaji thamani mazao ya kilimo na malighafi nyingine.
Aliiagiza SIDO kuweka mpango mkakati katika kila mkoa kwa mwaka 2025 hadi 2030 ili kuhakikisha kila mkoa unaanzisha viwanda vikubwa 3, vya kati 5 na vidogo 20 ukiwa na lengo la kuongeza thamani za mazao, uvuvi na ufugaji kwa baadhi ya changamoto walizonazo wanachi na kupunguza tatizo la ajira nchini. Alitoa mfano wa viwanda vilivyoanzishwa Morogoro hivi karibuni na namna vilivyoweza kuajiri idadi kubwa ya vijana. Aliongeza kuwa nchi zilizoendelea zina mafanikio makubwa kupitia viwanda vidogo hivyo mkakati huu utatafutiwa jina na siku ya ufunguzi utatangazwa. Alieleza kuwa kila mwaka vijana wapatao 64,000 huhitimu masomo yao vyuo mbalimbali kila mwaka na na wengi wao kukosa ajira, hivyo eneo kubwa linalotegemewa ni biashara, viwanda na kilimo.
Aliitaka mikoa pia kuainisha fursa mbalimbali zilizopo kwa ajili ya uwekezaji. Mfano mkoa wa Kigoma (samaki) ambapo sambamba na hiyo mashine mbalimbali zitakuwa zinatengenezwa kwa ajili ya kutengeneza vyakula vya samaki kama ilivyo kwenye vyakula vya mifugo. Lengo likiwa ni kila mkoa kushindana kibiashara kwa kuangalia mahitaji na fursa zilizopo ndani ya mikoa